“Kila kijiji kiwe na shule ya msingi na chekechea”

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi na darasa la awali.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Julai 8, 2023 baada ya kuweka Jiwe la Msingi ujenzi wa jengo la utawala Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara
“Tumeagiza kila kijiji kuwa na shule ya msingi na kila shule ya msingi iwe na darasa la chekechea ili watoto wote waanze kusoma chekechea kijiji hapohapo.” amesema Majaliwa.
Amewata maafisa elimu shule kupita kila shule ya msingi vijijini kujiridhisha kuna darasa la awali.
Amewataka na mabaraza ya madiwani kwenye eneo husika kusimamia utekelezaji wa agizo la kuwa na shule ya msingi kila kijiji na kuhakikisha linatekelezeka.
Majaliwa amesema ujenzi wa shule ya msingi kila kijiji ni mpango mkakati wa serikali kuimarisha miundombinu ya elimu katika kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu kama inavyopaswa.
Katika hatua nyingine amezitaka halmashauri kuhakikisha kunakuwa na shule ya sekondari kidato cha tano na sita.
“Kaeni pamoja mpange mnaweza kuchagua shule ipi ya sekondari muifanye kuwa shule ya kidato cha tano na sita kwa kuongeza miundombinu zaidi,” amesema.
Amewataka baraza la madiwani kusimamia kwa kukaa na ofisa elimu sekondari na mamlaka husika kuchagua shule na kuanzisha kidato cha tano na sita.