KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amos Makalla amesema aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wao, Abdulrahman Kinana amekifanyia chama mambo makubwa ikiwamo kukitoa ‘shimoni’ kuelekea mwaka 2015.
Amesema kutokana na kazi hiyo nzuri, chama hicho kitamuenzi na kumkumbuka katika historia kutokana na mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya CCM.
Makalla alisema hayo jana kwenye Kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC1 alipokuwa akihojiwa kuhusu Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Januari 18 na 19, mwaka huu mkoani Dodoma.
Alisema katika mkutano huo utakaokuwa na ajenda tatu, ajenda mojawapo ni ya kuchagua mrithi wa nafasi ya Kinana ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara aliyoitumikia kwa miaka miwili na nusu.
Makalla alisema Kinana ambaye aliomba kupumzika, amefanya mengi ya kukumbukwa tangu akiwa Katibu Mkuu wa CCM hadi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama Tanzania Bara na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
“Ni mtu ambaye amefanya kazi nzuri katika chama. Ana historia kubwa, amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu kwa muda mrefu sana. Amefanya kazi kubwa akiwa Katibu Mkuu wa chama na kukisaidia chama na kukifufua,” aliongeza Makalla.
Aliongeza kuwa miongoni mwa kazi kubwa aliyoifanya Kinana ni kupita katika ziara mikoani na kusikiliza kero za wananchi na kufanikiwa kukijenga chama kuanzia katika ngazi ya shina hadi ngazi ya taifa.
Akiwa Katibu Mkuu wa CCM, Kinana aliongoza operesheni ya kujenga chama kwa kuwawajibisha mawaziri ambao walikuwa wakisababisha chama kionekane hakiwajibiki na kuwaita ‘mawaziri mizigo’.
Kinana alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Aprili Mosi, 2022 baada ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kumchagua kwa kura za ndiyo 1,875 na kujiuzulu nafasi hiyo Julai 29, mwaka jana.
Moja ya mambo ambayo Kinana aliyaongoza katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti ni maridhiano kati ya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) maridhiano yaliyokuwa na mafanikio.
Mpaka anajiuzulu, Kinana ametumikia nchi katika nafasi mbalimbali zikiwamo jeshini ambako alishiriki katika Vita vya Kagera mwaka 1978 hadi 1979, serikalini na CCM.