Kinana aonya sheria  zinazoumiza wananchi

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameonya wabunge na  madiwani wasitunge sheria ambazo zinaumiza wananchi.

Amewataka  kabla ya kupitisha sheria ndogo ndogo wanapaswa kuandaa rasimu na kuipeleka  kwa wananchi, ili  waridhie.

Kinana amesema  kuna sheria nyingi  ngazi ya halmashauri zinalamikiwa na wananchi kwamba zinawakandamiza, huku akieleza hayo yote yanatokana na viongozi kutoshirikisha wananchi na kuridhia.

Advertisement

Akizungumza mkoani Mara  na wananchi wa Musoma Mjini kwenye viwanja vya shule ya Msingi Mkend,  ikiwa ni  muendelezo wa ziara yake ya  kukagua miradi ya chama hicho,  Kinana amesema  sheria nyingi zinazotungwa katika ngazi hizo hazitekelezeki kwa kuwa watu wanakuja kuzijua baada ya kukamatwa.

“Madiwani mnayo dhamana kubwa,  niwaombe, ili kupunguza malalamiko ya hizi sheria katika halmashauri zenu kabla ya kupitisha sheria mnapaswa kuandaa kwanza rasimu itakayopelekwa kwanza kwa wananchi wasome zile wanazoridhia  mzipitishe, wakisema hii hapana mbaya muache,” amesema  Kinana.

“ Hii sheria inataka kuletwa je mnaikubali wakikataa wanatakiwa kuiacha maana hao wananchi ndio wanaowachagua kwa kuwapigia kura lazima washirikishwe katika hizo sheria,” amesema.

Amesema katika kusimamia sheria kuna sheria, kanuni na taratibu kuna jambo lazima liende na utekelezaji wa sheria ambalo ni busara sio kila kitu ni sheria.

Amesema busara pia inapaswa kutumika si kila jambo wananchi wanakamatwa,  huku akihoji  kwani hizo sheria wanazotengeneza  hazina kipengele cha kusamehe?.

“Sio kila wakati ni kamata weka ndani kwani ninyi hamjui kusamehe,sheria yenu haina kifungu cha kusamehe hiyo sheria yenu ina adhabu peke yake mtu anachukua shughuli yake ndogo ameweka mahali anauza anakamatwa vitu vyote vinakusanywa na kuchukuliwa na mtaji unaishia hapo.

“Mtu ana bodaboda msije kusema amekuja Makamu Mwenyekitia amesema tupakie watu wawili au watatu hapana utakuta bodaboda imepakia watu wawili mtu na rafiki yake ukimsimamisha muambie sheria hairuhusu, ila kwa sasa hivi nenda sio unamchukua mwenye pikipiki na abiria unampeleka kwenye kituo cha polisi,” amesema.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan tangu alivyoingia madarakani amechukua hatua nyingi za maendeleo fedha zote amezitoa katika miradi ya maendeleo kwa kila mkoa.

Amesema kwa mara ya kwanza Rais Samia amepata fedha nyingi amefanya kila busara kuhakikisha kuna maendeleo katika miundombinu ya huduma za kijamii.

“Mimi nilikuja Mara nikiwa Katibu Mkuu kulikuwa na tatizo kubwa la maji leo hii hakuna, miaka yote nilipokuja hapakuwa na uwanja wa  ndege leo hii unajengwa na umefikia asilimia 50,”amesema Kinana.

Amesema, kazi kubwa waliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha mzunguko wa fedha unakuwa mzuri na mifuko yao kujaa fedha mkoani Mara.

Awali Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini (CCM), Vedasto Mathayo, alisema licha ya mafanikio makubwa waliyonayo wanakabiliwa na changamoto ya mzunguko wa fedha na baadhi ya viwanda kufungwa ikiwemo cha uvuvi.

Amesema, wamepatiwa mkopo kwa ajili ya vizimba vya uvuvi tatizo kubwa wanalolipata sasa ni mchakato wa Baraza la Taifa la Usimamizi Mazingira (NEMC) wamekuwa na masharti mengi kwa ajili ya kutoa nafasi hizo kuendelea na ujenzi.

Amesema pia, changamoto inayowakabili kwa sasa ni mzunguko mdogo wa fedha kwa wananchi unaochangiwa na vijana kukosa ajira na viwanda vingi vilivyokuwepo ikiwemo cha samaki kufa.

“Shida kubwa hapa ni mzunguko wa fedha kwa muda mrefu sasa na hii inatokana na viwanda vyetu vingi kufa ambavyo vilikuwa vinaajiri vijana wengi kwa mwananchi kupata hata sh 1000 ni changamoto,” amesema .

Katika kukabiliana na tatizo la ajira lipolipo mkoani hapo, aliishauri serikali kuangalia namna ya kujenga viwanda  vingi vya samaki na kuboresha vilivyokufa kwa kuleta mashine za kisasa

1 comments

Comments are closed.