Kinana: Vijeshi vidogo dogo visiwatoe kwenye reli

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amewataka wanachama wa Chama hicho kutoyumbishwa na maneno ya wapinzani na badala yake wajikite kwenye lengo.

Amesema lengo la Chama hicho ni kuendelea kushika Dola, hivyo wanajukumu kubwa la kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa kikamilifu.

Advertisement

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani Tabora, Kinana amesema “Nataka nizungumze jambo moja, ni kweli wenzetu ajenda zao ni za msimu , sisi ahadi zetu ni za kudumu, tuna mkataba na wananchi kupitia ilani,

“Tukitetereka na kutoka kwenye malengo tutapotea, jeshini vita ina kanuni 10 kanuni ya kwanza ukitaka kushinda inasema chagua lengo na ulishikilie usitoke nje ya lengo lako.

“Unapopigana, majeshi ya upande wa pili ili wakutoe kwenye lengo wanapeleka vijeshi vidogo vidogo pembeni kulia na kushoto wanapiga risasi ili wakutoe kwenye lengo lako, ukibabaika tu unakwenda kushoto, kulia, lengo linapotea.” Amesema

Amesema wana CCM wasitolewe kwenye lengo lao la kutimiza ahadi yao kwa wananchi, kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini vile vile, kutimiza mazungumzo waliyoyaanza ya maridhiano.

“Tembeeni kifua mbele, muisemee serikali yenu vizuri, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mengi mazuri, tunapomtaja taja Rais si kwa kumuadaha wala kumperemba tunampa sifa ambazo anastaili. ” Amesema Kinana

Amesema, Rais Samia kapeleka maendeleo kila Kata, kila wilaya, kila Mkoa kuna shughuli ya maendeleo inayoendelea na kwamba hayo mambo hayaji hivi hivi.

” Kipindi cha baba wa Taifa kulikua na mradi wa ‘Siasa ni Kilimo’ mradi mzima ulitumia sh milioni 60, Kilimo kwanza kipindi cha Kikwete ulitumia sh bilioni 3 leo tunazungumza kuimarisha Kilimo kwa sh trilioni 1 ili kuwatoa wakulima kwenye umaskini, sh trilioni 1 sio pesa ndogo. ” Amesema

Amesema, Rais Samia ametengeneza utaratibu mzuri wa makusanyo ya ndani na mwaka wa fedha ulioisha yamevunja rekodi tangu Tanzania ipate Uhuru, haijawahi kutokea

Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza kukusanya sh trilioni 1.9 kwa mwaka uliopita.

Aidha, Kinana amesema makusanyo hayo yamepatikana kwa sababu ya mpango mzuri, amekusanya mapato bila kashikashi, bila kutishana, bila kuwekana ndani, watu wamekubali kulipa Kodi na ada mbali mbali.

“Sio hivyo tu Rais amepata misaada mingi kutoka nje, Rais ameaminika, kutokana na kauli na vitendo vyake namna anavyoendesha serikali.” Amesema Kinana .

5 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *