Kinana: Watanzania waboreshewe mazingira biashara EA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amesema umefika wakati kwa mamlaka mbalimbali za serikali kuweka mazingira mazuri ya Watanzania kufanya shughuli za kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema hakuna sababu ya kuwapo kwa vikwazo vingi vitakavyosababisha wananchi kushindwa kutumia fursa zilizopo kwenye jumuiya hiyo huku akieleza kuwa Tanzania imebahatika kupakana na nchi nane jambo ambalo ni fursa kubwa kiuchumi.

Akizungumza na wana CCM na wananchi wa Kagera, Kinana alisema hivi karibuni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hatua ambayo imetanua fursa ya soko.

“Juzijuzi kulikuwa na mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakajiunga pale. DRC ukubwa wake ni mara mbili ya Tanzania, idadi ya watu wake ni mara mbili yetu sisi, mahitaji yao ni mara nne yetu, utajiri wao mara 20 ya sisi sasa kitu gani unataka zaidi ya hilo, ni fursa kubwa,” alisema.

Kinana alisema kazi ya wabunge pamoja na viongozi ni kuelimisha wananchi kuhusu fursa zilizopo na namna Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inavyotoa nafasi kwa watu kufanya shughuli zao na biashara ya mipakani.

“Mtu anapeleka bidhaa zake Uganda, unamuuliza unaenda wapi? Wakiwauliza wajibuni naenda Dar es Salaam, wafanyabiashara wa kigeni wakija cha kwanza anaulizwa unaondoka lini?”

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuondokana na sheria zote zinazoleta vikwazo katika shughuli za wananchi na kuwa kazi yake na viongozi wengine ni kumpa moyo kwa kumuambia kuwa njia anayokwenda ni sawa.

Alisisitiza kwamba baada ya kumaliza ziara yake atakaporudi atakwenda kumwambia Rais Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kwamba wananchi wa Mkoa wa Kagera wamemwambia  apeleke bungeni sheria za hovyo ili zifutwe.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button