Kiruswa: biashara ya makaa ya mawe ni utajiri

Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa amebainisha kuwa, biashara ya Makaa ya Mawe inatarajia kuleta tija kwa Watanzania kutokana na uhitaji mkubwa wa madini hayo ndani na nje ya nchi.

Dk. Kiruswa ameeleza hayo Novemba 12, 2022 wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma alipotembelea mgodi wa uchimbaji wa Makaa ya Mawe wa Ruvuma Coal Ltd ili kujionea shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika mkoa huo.

Ameeleza kuwa, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayovutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani kuja kuwekeza na kufanya biashara ya madini mbalimbali yakiwemo Makaa ya Mawe.

Advertisement

Aidha ameongeza, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa Makaa ya Mawe kutoka kwenye migodi hususan barabara ya kuelekea mkoani Mtwara ili kusafirisha Makaa ya Mawe hayo katika bandari.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo amesema, kutokana na uwepo wa migodi imesaidia wilaya hiyo kupata faida nyingi katika kutekeleza shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga amesema Makaa ya Mawe yanahitajika kwa wingi duniani kwa sasa.

Amesema Serikali itumie fursa hiyo kuhakikisha wilaya inapata faida ya uwepo wa migodi kwa kutoa ajira na kuleta maendeleo kwa jamii zinazozunguka mgodi hiyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *