ARUSHA: JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kushirikiana na Kenya na Uganda zimeanza mchakato wa kuboresha kituo cha mpakani cha Lwakhakha kwenye mpaka wa nchi hizo mbili ili kiwe Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP).
Kuanzishwa kwa kituo hicho ni mkakati wa kupunguza msongamano katika vituo kama hicho vya Busia na Malaba.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Mwandamizi Idara ya Mawasiliano ya Umma na Masuala ya Umma, Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Arusha, Simon Owaka katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
SOMA: Ruto ataka migogoro ya mipaka kutatuliwa
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa kubadilishwa kwa mpaka wa Lwakhakha kuwa Kituo cha kutoa huduma kwa pamoja mpakani kunalenga kurahisisha taratibu za forodha, kupunguza muda wa uidhinishaji wa bidhaa na magari na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za serikali za Kenya na Uganda katika mpaka huo.
Uboreshaji huo pia umetajwa kuwa utasaidia kupunguza msongamano wa magari kutoka vituo vya mpakani vya Malaba na Busia na kuongeza biashara katika ukanda wa Kaskazini na kuboresha usalama wa mipakani.
Pia taarifa hiyo ilisema mpango huo ni dhamira ya EAC katika kukuza ushirikiano mipakani kati ya nchi hizo mbili, hivyo Kituo cha Lwakhakha kitazisaidia Kenya na Uganda kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa manufaa ya wafanyabiashara na jamii za mpakani.
Mhandisi Mkuu wa Ujenzi wa Sekretarieti ya EAC, Godfrey Enzama amesema upandishaji hadhi wa kituo cha mpakani cha Lwakhakha na kuwa OSBP ni sehemu ya upembuzi yakinifu wa kilometa 256 wa mradi unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Enzama amesema hayo alipozungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia sekta za miundombinu, uzalishaji, jamii na siasa, Aguer Malueth wakati wa ziara ya kukagua upembuzi yakinifu unaoendelea wa Barabara ya Kimataifa ya Mwendokasi ya Kisumu-Kisian-Busia/ Kakira-Malaba-Busitema-
SOMA: https://www.eac.int/
Busia. Alisema EAC inashirikiana kwa karibu na wadau husika ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa mpaka huo unafanikiwa. “Juhudi hizi za ushirikiano zinaakisi dira ya pamoja ya kukuza uwezeshaji wa biashara, usalama wa mpakani na ushirikiano wa kikanda katika Afrika Mashariki,” alisema Enzama.
Alisema kuiboresha Lwakhakha kuwa OSBP kutaimarisha uongezaji wa thamani na kukuza mauzo ya nje yenye thamani kubwa kwenye masoko ya kikanda na kuongeza ajira miongoni mwa vijana waishio maeneo ya mpakani.