Kivumbi Samia Women Super Cup 2025
VUMBI litatimka wakati wa mashindano ya Samia Women Super Cup iliyopangwa kufanyika mapema mwezi ujao ikihusisha klabu za JKT Queens, Simba Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Katika droo iliyofanyika leo michuano hiyo itaanzia nusu fainali huku Simba Queens itavaana na JKT Tanzania katika nusu fainali ya kwanza wakati Yanga Princess itakabiliana na Fountain Gate.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, mashindano hayo yataanza rasmi Machi 4.

Amesema mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itachezwa machi 6, huku fainali ikifanyika Machi 8, siku ambayo pia itakuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake.



