Kiwanda cha mwani kumkomboa mkulima

Kiwanda cha mwani kumkomboa mkulima

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amesema ujenzi wa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani zao la mwani ni mkombozi kwa wakulima wa kilimo hicho.

Abdullah alisema hayo huko Chamanangwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati alipofanya ziara kuangalia ujenzi wa kiwanda hicho ambao unafanywa na kikosi cha KMKM.

Alisema azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuona kilimo cha mwani kinapiga hatua kubwa za maendeleo na kuwa mkombozi kwa wakulima ambao kwa asilimia 90 ni wanawake.

Advertisement

Alisema kilimo cha mwani ni sehemu ya vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo katika fedha za Covid-19 serikali imetenga Sh bilioni 49 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuingia katika kilimo cha mazao ya baharini.

Alisema katika kuona zao la mwani ni muhimu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunda kampuni ya mwani kwa ajili ya kukiendeleza na kukisimamia kilimo hicho kuweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Mapema Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwani Zanzibar, Dk Masoud Rashid Mohamed alisema ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka 2023 kikiwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya tani 30,000 kwa mwaka.

Alisema ujenzi wa kiwanda hicho kwa kiasi kikubwa kitaongeza hamasa za wakulima kuimarisha kilimo cha mwani kwa sababu kitaongeza thamani ya usarifu na bei ya mwani sokoni.

Alisema miongoni mwa kilio kikubwa cha wakulima wa kilimo cha mwani ni bei ndogo ambayo haiendani na hali halisi ya thamani ya zao hilo ambalo harakati zake ni kubwa.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban aliwataka wakulima wa kilimo cha mwani kujipanga zaidi ikiwemo kuimarisha mashamba yao kwa ajili ya kupata kipato kikubwa.

Alisema ujenzi wa kiwanda hicho kwa tafsiri ya moja kwa moja ni kwenda kuimarisha kilimo cha mwani na kuongeza thamani kwa wakulima kwa ajili ya kupata kipato kikubwa.

”Ujenzi wa kiwanda hiki ni ujumbe kwa wakulima wa mwani kwenda kuongeza juhudi zaidi za kuimarisha kilimo hicho ili kupata mwani mwingi utakaoweza kwenda kiwandani na kusarifiwa bidhaa mbalimbali,” alisema.