Kizimbani akidaiwa kujipatia Sh Bil 5 kwa njia ya udanganyifu

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jatu Public limited, Peter Gasaya (32), mkazi wa Dar es salaam amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kujipatia fedha tasilimu Sh 5,139, 865,733.00 kwa njia ya udanganyifu.

Mshitakiwa amesomewa shitaka leo na wakili wa serikali Tumaini Mafuru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mery Mrio.

Mafuru alidai kuwa katika terehe isiyofahamika kati ya Januari mosi na  Desemba 31, 2021 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jatu Public Limited, alijipatia Sh 5,139,865,733.00 kutoka  Saccos ya Jatu, akijinasibu kukizalisha kiasi hicho cha fedha kwa kuwekeza fedha katika kilimo cha faida wakati akijua  si kweli.

Awali Mafuru alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mshitakiwa alikana shitaka na kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 11, 2023, huku mshitakiwa akiendelea kubaki rumande kwa sababu mahakama hiyo haina Mamlaka ya  kumpa dhamana kutokana na kiwango cha dhamana kuzidi Sh milioni 300.

 

Habari Zifananazo

Back to top button