Kizimbani kwa tuhuma za kutaka kumuua Ofisa Utumishi

JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora limewafikisha mahakamani watu watatu wakiwemo watumishi wawili na mkulima wakidaiwa kujaribu kumuua Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Mussa Abdallah (38).

Katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga, mwendesha mashitaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga, Eda Kahindi alitaja washitakiwa hao kuwa ni Jahulula Edward Jahulula (41), mkazi wa Mtaa wa Nkokoto Kata ya Igunga mjini aliyekuwa Kaimu Ofisa Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Washitakiwa wengine ni Emmanuel Ikandiro (48) mkazi wa Mtaa wa Masanga Kata ya Igunga mjini ambaye ni mhandisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Masanja Bukwimba (43), mkulima wa Kata ya Mbutu iliyopo Wilaya ya Igunga.

Kweyamba aliieleza mahakama kuwa washitakiwa hao watatu wanakabiliwa na shitaka la kujaribu kuua.

Alisema Machi 10, mwaka huu saa moja na dakika 45 usiku katika Mtaa wa Mwayunge Kata ya Igunga mjini washitakiwa wakiwa na nia ovu walijaribu kumuua Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Mussa Abdallah (38) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni wakati akiwa amepumzika nyumbani kwake baada ya kutoka kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Kweyamba alidai kuwa washitakiwa wote watatu walitenda kosa hilo kinyume na kifungu 211 (a) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2022.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 25, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button