Kombe la Mkuu wa Majeshi Julai 20

DAR ES SALAAM – MASHINDANO ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF 2024) yanatarajiwa kuanza Julai 20 huku mechi ya ufunguzi ikitarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Mashindano hayo, Brigedia Jenerali Said Said, alisema kaulimbiu ya michuano hiyo ni ‘Ushindi ni Heshima’.

Alibainisha kuwa wamejiandaa vyema na kwamba mashindano hayo yatakuwa ya kuvutia, huku akitaja lengo la mashindano hayo kuwa ni kuboresha afya na kujenga umoja na mshikamano wa wanajeshi.

“Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi yameanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha wanajeshi wote nchini kutoka kila Kamandi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ambao ni maafisa, askari pamoja na watumishi wa umma wanaofanya kazi jeshini ili kuendelea kuboresha afya na kujenga umoja, ushirikiano na mshikamano katika utendaji wa majukumu ya kila siku,” alisema Said.

SOMA: Waziri Mkuu ashiriki Great Ruaha Marathon

Said alisema mashindano yatahusisha timu za michezo mbalimbali kutoka vikosi vyote chini ya Makao Makuu ya Jeshi, Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Anga, Jeshi la Wanamaji, Jeshi la Akiba na Jeshi la Kujenga Taifa. Jumla ya timu tisa zitashiriki kwenye michuano hiyo itakayohitimishwa Julai 30, mwaka huu.

Timu hizo ni za michezo ya mpira wa miguu wanaume, netiboli kwa wanawake, mpira wa mikono kwa wanaume na wanawake, kikapu kwa wanaume na wanawake, ngumi kwa wanaume na wanawake na kulenga shabaha kwa wanaume na wanawake.

Habari Zifananazo

Back to top button