Kongamano la sayansi, teknolojia kufanyika Juni Dar

KONGAMANO la mwaka kitaifa na maonesho ya sayansi, teknolojia na ubunifu linatarajia kufanyika jijini Dar es Salaam Juni 14-16 mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Costech, Dk Amos Nungu amesema litawakutanisha wanasayansi, watafiti, wabunifu, watunga sera na wananchi kujadili kazi za sayansi, teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya nchi na kwamba wamemualika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.

Dk Nungu ameeleza lengo la kongamano hilo ni kuwezesha watafiti, wanasayansi na wabunifu kukutana na watunga sera kujadili matokeo ya tafiti na bunifu nchini yanavyochangia kutengeneza sera na kujenga Taifa linaloendeshwa na sayansi, teknolojia na ubunifu.

“Malengo mengine ni kuishauri serikali na vyombo vyake kupitia matokeo ya kitafiti za kisayansi na maendeleo ya teknolojia, pia watafiti, wabunifu na wavumbuzi kupata fursa ya kupokea mwelekeo wa sera kutoka kwa viongozi wa kitaifa na Waziri mwenye dhamana,” amesema.

Amesema katika kongamano hilo Rais Samia atatoa tuzo kwa watafiti, wavumbuzi na wabunifu bora ili watambulike kitaifa.

Kwa maelezo ya Dk Nungu kongamano hilo litawezesha watafiti, wavumbuzi na wabunifu wa ndani ya nchi kukutana na wenzao kutoka nje ili kujenga mahusiano ya kibiashara na utafiti.

Habari Zifananazo

Back to top button