Korea kusaidia Z’bar utalii wa mikutano

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali yake imejipanga kutekeleza utalii wa mikutano kwa kujenga majengo na kumbi za mikutano ili kuvutia wageni kutoka nje kuja kufanya mikutano Zanzibar.

Dk Mwinyi alisema hayo jana wakati alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari ukiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kila mwisho wa mwezi kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu Zanzibar.

Alisema tayari ameshazungumza na Serikali ya Korea ambayo imekubali kuisaidia Zanzibar katika ujenzi wa majengo hayo utakaofanyika Kilimani na kuongeza kuwa wenyeji wa maeneo hayo watalipwa fidia na kujengewa majengo mengine katika sehemu watakayopendekeza.

Dk Mwinyi alisema uchumi wa Zanzibar unategemea utalii ikizingatiwa kuwa duniani kote sasa hivi utalii wa namna hiyo ni mkubwa na unafanya vizuri.

Alisema katika utalii huo wageni wanapomaliza kufanya mikutano yao wanatembelea fukwe za bahari kupata mandhari safi pamoja na kutembelea Mji Mkongwe kujionea vitu mbalimbali hivyo majengo ya mikutano yanajengwa karibu na bahari na katikati ya mji.

“Utalii kwa Zanzibar ndio moyo wa uchumi wetu, tupende tusipende kwani asilimia 30 ya mapato ya serikali yanatokana na utalii, tukiongeza utalii wa namna hiyo mpya tutaongeza mapato ya serikali na nchi kwa ujumla,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema utalii wa namna hiyo hausaidii serikali peke yake bali unasaidia kila mtu kwa sababu hakuna kipindi mtu atasema hana kazi kwani misimu ya kukosekana watalii, mradi huo ni njia ambayo inaweza kuwavutia watalii kuja kufanya mikutano yao na kutembelea vivutio.

Aidha, Dk Mwinyi alisema serikali yake pia ina mpango wa kukabidhi Bandari ya Malindi kwa mwekezaji wa kimataifa ili aongeze ufanisi wa bandari hiyo ambaye atasaidia serikali kufikia malengo yake katika bandari.

Dk Mwinyi alisema pindi mwekezaji huyo atakapopatikana, moja ya makubaliano atakayoingia na serikali ni kupunguza kabisa muda wa kupakia mizigo katika meli moja kutoka siku saba hadi kufika siku mbili tu hali itakayochangia kuongeza ufanisi katika bandari.

Alisema ili kuwavutia wateja wa bandari hiyo ambao wamekimbilia katika Bandari ya Mombasa, serikali inajenga Bandari Kavu katika eneo la Fumba ili kuchukua makontena ya Zanzibar kutoka Mombasa kwa sababu kilichosababisha wakimbilie huko kimeshaondolewa.

Katika hatua nyingine, Dk Mwinyi alionesha kukerwa na watu wanaokiuka maadili ya Kizanzibari na kuagiza hatua zichukuliwe dhidi ya watu wanaokiuka tamaduni za nchi na kufuata mila, desturi na tamaduni zinazokinzana na maadili ya nchi.

Dk Mwinyi aliwaambia wanahabari kuwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaendelea kufanyiwa kazi ambapo hadi sasa viongozi kadhaa wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kishera.

Habari Zifananazo

Back to top button