Korosho; ‘dhahabu’ inayofanya mageuzi ya kiuchumi Kusini

KWA miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mageuzi makubwa yamefanywa katika sekta ya kilimo kikiwemo kilimo cha korosho mikoa ya Kusini.
Hatua hiyo imeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa mwananchi mmojammoja, jamii na taifa kutokana na uwekeza mkubwa uliofanywa na serikali kuwezesha ruzuku za uhakika na kwa wakati katika pembejeo kwenye zao la korosho.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred anasema serikali imewekeza kimkakati kuimarisha kilimo cha korosho na mageuzi hayo yamedhihirika hata kwa wakulima moja kwa moja.
Anasema jumla ya ruzuku katika miaka minne kuanzia 2021/2022 hadi 2024/2025 katika zao la korosho ni Sh bilioni 626 na kila mwaka imekuwa ikiongezeka. Anasema mwaka 2021/2022 ilikuwa Sh bilioni 59.4, mwaka 2022/2023 Sh bilioni 96.3, mwaka 2023/2024 Sh bilioni 189.3 na mwaka 2024/2025 Sh bilioni 281.
Kwa mujibu wa CBT, upande wa mbolea msimu huu wa mwaka 2025/2026 lengo la serikali ni kusambaza salfa tani 40,000 na viuatilifu vya maji lita 2,000,000 ambapo makadirio ya gharama ya pembejeo hizo ni Sh bilioni 280. Usambazaji wa pembejeo kwa kipindi hicho umewezesha msimu ulioisha 2024/2025 uzalishaji wa korosho ufikie tani 528,000 na lengo la msimu ujao wa 2025/2026 ni tani 700,000.
Francis anasema faida kubwa ya pembejeo za ruzuku kwa wakulima ni uhakika wa kupata pembejeo za ruzuku ya asilimia 100, hivyo kuwawezesha kudhibiti visumbufu (wadudu na magonjwa) na kuongeza uzalishaji (tija) jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa kipato miongoni mwa wakulima.
Anasema CBT imekuwa ikitoa elimu ya kanuni za kilimo bora cha korosho katika miaka yote na kuchangia mafanikio hayo. “Katika msimu wa 2025/2026 ili kuongeza ufanisi zaidi na kusongeza huduma za Bodi ya Korosho kwa wakulima, Bodi imeajiri vijana 500 kupitia mpango wa Wizara ya Kilimo wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT),” anasema.
Anasema vijana hao wamejengewa uwezo kusimamia shughuli za usimamizi katika ngazi ya kata pamoja na kutoa elimu ya kanuni za kilimo bora cha korosho. Ili kuendeleza mapinduzi ya kilimo cha korosho, anasema vijana hao 500 wote wamepatiwa pikipiki na vishikwambi kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wao kwa kuwahudumia wakulima ipasavyo kama ilivyokusudiwa.
Kimsingi, korosho ni moja ya mazao ya kimkakati ya biashara Tanzania hivyo, nguvu hizo za uwekezaji zinachochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii katika mikoa inayolima zao hilo hasa ya Kusini ambako hilo ni zao lao kuu la biashara.
Tafsiri ya mageuzi na mapinduzi haya ni kuendeleza wito aliotoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hivi karibuni alipofanya ziara mkoani Mtwara. Akiwa huko pamoja na mambo mengine alisisitiza wakulima kujipanga kuuza korosho iliyobanguliwa ili kuongeza tija badala ya kuuza korosho ghafi.
Waziri mkuu wanasema serikali imedhamiria kufufua viwanda vya kubangua korosho. Anasema lengo la serikali ni kuongezea thamani zao hilo kwa mkulima mmojammoja na hata taifa kwa ujumla ili kutowakosesha wakulima na nchi faida.“Wakati wa kubadilika umefika, tutumie fursa hii kujenga viwanda vya kubangulia korosho na kuwawezesha wakulima kubangua na kuuza katika masoko ya nje na ndani,” anasema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Rais Samia Suluhu Hassan anahitaji kuona Tanzania inauza korosho zilizobanguliwa nchini badala ya kuuza korosho ghafi nje. Kilo moja ya korosho iliyobanguliwa ni takribani Sh 13,000na korosho ghafi ni Sh 2,000.
Anabainisha kuwa, kilogramu nne za korosho ghafi zikibanguliwa hupatikana kilogramu moja ya korosho iliyobanguliwa hivyo kuna mapato yanayopotea kwa kuuzwa korosho ghafi. Serikali imefanya kwa sehemu kubwa, uwekezaji wa mabilioni ya fedha kwenye pembejeo za ruzuku unadhihirisha dhamira yake kuinua kilimo cha korosho.
Aidha, anatoa mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda vya kubangua korosho. Mwito huo pia umekuwa ukitolewa na viongozi wa serikali kila kukicha.
Kwa msingi huo, wakati ambapo mchakato wa kufufua viwanda vya kubangua korosho vilivyokufa ukiendelea, huku mazingira ya uwekezaji yakiendelea kuwa rafiki kwa kanuni, sheria na taratibu bora, wenye viwanda wawape nafasi wakulima kubangua korosho zao na kuwatoza gharama za ubanguaji zisizoumiza ili wapate faida na kujiongezea kipato.
CBT nayo iendelee kuweka nguvu katika usimamizi wa zao hili ili lisiporomoke, bali liendelee kukua katika soko la dunia na ubora wa korosho ya Tanzania uendelee kusimamiwa ili zao hili liilishe si Afrika, tu bali dunia nzima. Hivi karibuni CBT kupitia programu ya BBT ilitoa pikipiki 67 kwa maofisa ugani kuboresha huduma za kilimo cha korosho Masasi mkoani Mtwara.
Hatua hii inapaswa kuendelea ili wakulima si Masasi peke yake, bali hata mikoa yote inayolima zao hili la kimkakati wafikiwe, wahudumiwe kwa ufanisi zaidi hasa maeneo ya vijijini yenye changamoto za miundombinu ya usafiri.
Hatua hiyo ambao ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha sekta ya kilimo cha korosho kupitia uwezeshaji wa rasilimaliwatu na vifaakazi, unapaswa kuungwa mkono pia kwa wanaokabidhiwa vifaa kuhakikisha wanavitumia
kwa malengo husika ili tija ipatikane.
Mikoa inayotegemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 80 kikiwemo cha korosho kama ya Kanda ya Kusini, nguvu kubwa ielekezwe katika uwekezaji wa elimu kwa wakulima, kilimo cha kisasa cha kibiashara kinachozingatia mabadiliko ya kila wakati ya teknolojia. Francis anasema CBT imejipanga kusimamia uendelezaji wa kilimo cha korosho kwa teknolojia bunifu na cha kisasa na hii ndio maana halisi ya kilimo biashara.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwahi kusema dhamira na malengo ya sekta ya kilimo nchini ni kujitosheleza kwa chakula, kuuza soko la ndani na nje kwa kuzingatia viwango vya ubora wa kimataifa ambavyo tayari bidhaa nyingi za Tanzania ikiwemo korosho zinavyo.
Hii ina maana kuwa, ‘dhahabu hii ya Kusini’ inayoleta mapinduzi ya kiuchumi hivi sasa kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali, uendelee kusimamiwa kwa maslahi mapana ya nchi.