BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kesho ni ukomo wa kutumia noti za zamani.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, BoT imetangaza kuwa ubadilishwaji wa noti za zamani ulianza Januari 6, mwaka huu, kesho ni mwisho na
matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania.
“Baada ya tarehe hiyo mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote nchini na benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko,” ilitangaza BoT jana.
Noti zinazoondelewa kwenye mzunguko ni Sh 20, Sh 200, Sh 500, Sh 1,000, Sh 2,000, Sh 5,000, Sh 10,000 zilizochapishwa kati ya mwaka 1985 hadi 2003 na noti ya Sh 500 ya mwaka 2010.
Wananchi wanapaswa kuzipeleka kwenye matawi ya BoT au benki yoyote ya biashara nchini na kubadilishiwa kupewa malipo ya thamani sawasawa na kiasi walichowasilisha.
Awali, BoT ilisema uamuzi wa kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za Shilingi ya Tanzania zilizoidhinishwa kutumika na benki hiyo mwaka 1985 hadi 2003 na noti ya Sh 500 iliyoanza kutumika mwaka 2010, halina athari za kiuchumi.
Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu wa BoT, Ilulu Ilulu alisema noti zinazoondolewa hazijashuka thamani na kinachofanyika ni utaratibu wa kawaida wa benki kwa mujibu wa sheria kufanya hivyo inapoona kuna haja ya kufanya hivyo.
Ilulu alisema Dar es Salaam kuwa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, Sura ya 197 kifungu cha 26 imeipa BoT mamlaka ya kuchapisha noti na kuzisambaza nchini.
Alisema kifungu cha 27 (2) cha sheria hiyo kinaipa mamlaka BoT kuzitangaza noti hizo kabla ya kuziingiza kwenye mzunguko na kifungu cha 28 (2), (3) kimeipa mamlaka ya kusitisha uhalali wa fedha itakazoziainisha na pia inapaswa kuwapa wananchi muda maalumu wa kuzibadilisha kabla ya kusitisha,” alisema Ilulu.
Ilulu alisema kinachofanywa na BoT si jambo geni na hakuna mpango wa kutoa matoleo mapya ya noti.
“Tunatumia noti zilizochapishwa mwaka 2010 ndio toleo letu linaloendelea kutumika hadi sasa na kama ni kuchapisha noti tutaendelea kuchapisha hizi hizi za mwaka huo, hakuna toleo jipya kwani tuliyonayo bado ni bora na hatukusudii kutoa mapya,” alisema.
Aliongeza: “Benki Kuu imetekeleza zoezi la aina hii mara nne nchini, moja ilikuwa mwaka 1977 kwa kuondoa noti ya Shilingi 100 iliyochapishwa mwaka 1966 hadi 1977”.
Uondoaji mwingine ulifanywa mwaka 1979 kwa kuondoa noti ya Sh 10 na Sh 20 zilizochapishwa kati ya mwaka 1966 hadi 1979.
Pia, mwaka 1980 BoT iliondoa noti ya Sh tano na Sh 20 iliyochapishwa kati ya mwaka 1966 hadi 1980 na zoezi la mwisho lilikuwa mwaka 1995 ambapo waliondoa noti ya Sh 50 na Sh 100 zilizochapishwa kati ya mwaka 1979 hadi 1995.