Latra yataka watumiaji reli kuzingatia usalama
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa anatarajiwa kuzindua wiki ya usalama wa reli nchini iliyoanza jana hadi Oktoba 16, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Habibu Suluo, iliwataka watumiaji wa huduma za reli na wananchi kuwa waangalifu wanapotumia huduma za reli.
Aliwataka wachukue tahadhari za kiusalama wakati wote wanapotumia huduma za reli wakiwa kwenye vituo vya reli, ndani ya mabehewa na wanapopita kwenye maeneo ya reli.
“Ni muhimu kufahamu kwamba treni zinakwenda kwa mwendo kasi na zinaweza kukawia au kushindwa kusimama ghafla inapotokea dharura. Hivyo basi ni wajibu wa kila mwananchi kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha,” ilisema taarifa.
Ilielezwa kuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), watahakikisha kuwa huduma za usafiri wa reli nchini zinatolewa kwa ubora na usalama kwa watumiaji na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Latra iliwasisitiza wananchi wanaoishi maeneo inakopita reli na Watanzania wote kwa ujumla, kutumia wiki ya usalama wa reli kukumbushana umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya reli pamoja na mazingira kwa maendeleo ya nchi.
Imewataka kuunga mkono juhudi za serikali katika uwekezaji mkubwa unaoendelea ili kuboresha miundombinu ya reli na kukuza uchumi wa Tanzania.
Maadhimisho ya wiki ya usalama wa reli mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: Chukua Tahadhari, Treni Zina Mwendo Wa Haraka, Ni Hatari.