Lemutuz kuagwa leo Dar

MWILI wa mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, John Malecela, William Malecela maarufu kwa jina la Lemutuz unatarajiwa kuagwa leo katika Viwanja ya Karimjee, Dar es Salaam.

Mwili wa Lemutuz unatarajiwa kuzikwa kijijini kwa wazazi wake, Mvumi mkoani Dodoma.

Rafiki wa Lemutuz, Kinjekitile Kingunge alikaririwa akisema kuwa rafiki yake alikuwa na tatizo la moyo kwa muda mrefu na hadi juzi usiku alikuwa vizuri.

“Ndugu yetu alikuwa na matatizo ya moyo lakini alikuwa yuko vizuri tu, hadi jana usiku (juzi) alikuwa mzima, ghafla leo alfajiri alijisikia vibaya akawahishwa hospitali ya Mnazi Mmoja ambako ni jirani na kwake kisha akahamishiwa Muhimbili, lakini ndiyo hivyo ametutoka”.

Mmoja wa wanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Kolimba Malecela alisema kifo cha Lemutuz kimewashtua, kimewaumiza na ni pigo kwa familia.

“Familia kama familia bado kila mmoja yupo na shock (mshtuko), kila mmoja anavuta pumzi kwa namna yake ili aweze kujituliza kidogo kisha tuone wakubwa sasa wa familia wanasema nini,” alisema Kolimba.

Lemutuz alikuwa maarufu katika mitandao akimiliki blog ya Lemutuz, televisheni ya mtandaoni ni ya Lemutuz Online na kurasa kwenye mitandao hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button