LEO ni kumbukizi ya miaka miwili tangu afariki dunia Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Dk Magufuli aliaga dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam na akazikwa Machi 26 nyumbani kwake Chato mkoani Geita. Alizaliwa Chato Oktoba 29, 1959.
Wakati akitangaza msiba huo, Makamu wa Rais wakati huo na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan alisema Dk Magufuli alifariki dunia kutokana na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.
Machi 19, 2021, Samia aliapishwa katika Ikulu ya Dar es Salaam kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Machi 22 wakati wa mazishi ya kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Rais Samia alisema Dk Magufuli alimuandaa vizuri kuongoza nchi hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi.
Alisema ataendeleza pale alipoishia Dk Magufuli na atahakikisha anafikisha nchi mahali alipotamani ifike.
“Tutahakikisha tunafanikisha na kufikisha Tanzania mahali alipotaka Tanzania ifike,” alisema Rais Samia na kuongeza:
“Tumepikwa, tumeiva haswa na tumeiva sawa sasa, tupo tayari kuendeleza kazi alizoacha na kufikia pale alipotamani kufika kwa nguvu, kasi na ari ile ile.”
Alisema taifa limepoteza kiongozi jasiri, mchapakazi, hodari, imara, mtetezi wa wanyonge, mwanamwema wa Afrika na mwanamageuzi na mtumishi wa wote.
Rais Samia alisema Dk Magufuli alisimamia rasilimali za umma na kutekeleza miradi ya kimkakati akilenga kujenga Tanzania ya viwanda kwa kufungamanisha na ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu, maji na miundombinu.