LHRC, TAWLA wahimiza wosio kusaidia watoto nje ya ndoa

WADAU wa sheria na haki za binadamu wamesema wosia unaweza kuwasaidia watoto waliozaliwa nje ya ndoa wapate mgao wa sehemu ya mali za wazazi wao.
Hivi karibuni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alitoa mwito kwa jamii ione umuhimu wa kuacha wosia ili wajane na yatima wasidhulumiwe mali.
Dk Mpango alisema hayo katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma wakati yeye na mkewe, Mbonimpaye Mpango waliungana na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuaga na kuusindikiza mwili wa aliyekuwa mtumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Emmanuel Majanja.
“Inapowezekana ni vema sana kuacha hata maandishi mapema kwamba mimi siku zangu zikifika basi vitu hivi ambavyo nimechuma pamoja na mwenzangu mgawanyo wake upo hivi, hivi, hivi,”alisema Dk Mpango na kuongeza:
“Na mkavipeleka kwa wanasheria au benki vikahifadhiwa. Sijui binadamu tunakuwaje, tunakuwa na hulka za kunyang’anya hata mali za watoto yatima, sio kitu kizuri hata kidogo”.
Mkuu wa Programu Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Mary Richard alisema bila kujumuisha watoto wa nje ya ndoa katika wosia, sheria zinaweza kusumbua wakati wa kushughulikia mirathi.
Mary alisema hakuna mtu wala taasisi inaweza kwenda kinyume na wosia wa marehemu kwa kuwa hata sheria za urithi, dini na mila hazitambui mgao wa mali za marehemu kwa watoto wa nje ya ndoa.
Alisema sheria ya urithi inatambua warithi ni baba au mama, watoto wa kuzaa, watoto wa kuasili na wategemezi ambao bila kujali umri wao walikuwa wakimtegemea mzazi aliyeaga dunia.
Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema watoto wengi wa nje ya ndoa wanakosa haki ya kupata mali za wazazi wao kwa kuwa wanatengwa na ndugu na jamaa wakati wa kugawa mali za marehemu.
“Watoto wa nje ya ndoa wakijumuishwa kama warithi halali wa mali za baba au mama katika wosia watapata na kufaidi mali za mzazi wake sawasawa kama walivyo watoto waliozaliwa ndani ya ndoa,” alisema Massawe.
Alihimiza vyombo vya habari viendelee kuelimisha wananchi kuhus umuhimu wa kuandika wosia na akasema hata migogoro ya kugombea maiti inasababishwa na kutoandika wosia.
Massawe alisema wosia ni muhimu kwa kuwa unajenga, kuendeleza na kuleta amani katika familia hata kama mhimili unapokosekana na usipoandikwa familia inaweza kupitia wakati mgumu na wakati mwingine kusambaratika.
Aliihimiza jamii iache mtindo wa kuficha taarifa za mali zilizopo nje bila familia kwa kuwa hakuna mwenye uhakika na kesho yake.
Alisema kama mmiliki akiificha familia yake na akafariki dunia hazitokuwa na msaada kwa warithi wake lakini akiandika wosia zingewanufaisha.
Meneja wa Masoko na Elimu kwa Umma wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Josephat Kimaro alisema mtoa wosia anaweza kukataa hata wanawe wasiwemo wakati wa kugawana mali lakini lazima atoe sababu katika wosia inayoeleza kwa nini hawastahili kupata mgao wao.
Kimaro alisema mtoa wosia anaweza kumkataa mtoto asiwe sehemu ya warithi wake kwa sababu mbalimbali kama vile kutomtunza wakati wa mapito fulani, hamjulii hali, ana tabia mbaya na kadhalika.