Longido watoa mil 198/- vijana kujikwamua

ARUSHA: JUMLA ya Sh milioni 198 zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha kwa ajili ya vijana kujikwamua kiuchumi na kuacha kutegemea ajira serikalini.
Hayo yalisemwa na Ofisa Vijana Wilaya ya Longido Mussa Kabla wakati wa kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido,Dk Steven Kiruswa kufungua kongamano na mafunzo ya ajira mbadala kwa vijana 200 wa wilaya hiyo lengo ni kutaka vijana kujiajiri na kuacha kutegemea ajira serikalini.
Kabula alisema kiasi hicho cha fedha kimetolewa kwa vikundi 20 vya vijana Longido kwani kila kikundi kina vijana watano na kabla ya kupewa fedha hizo walikuwa na dokezo la mradi wa biashara watayofanya na kwa kiasi kikubwa halmashauri inazingatia hilo.
Alisema katika bajeti ya mwaka 2024 hadi julai mwaka huu halmashauri ya Longido imetenga kiasi cha Sh milioni 390 kwa vijana,wanawake na walemavu na kila jinsi imelekezwa na kufundwa kabla ya kukopeshwa nini wanapaswa kufanya kwa maslahi yao.
Naye Kiruswa alisema kuwa lengo la kongamano hilo la tatu kufanyika wilayani Longido ni kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuacha fikira za kutegemea ajira serikali kwani ajira serikalini ni janga la Kidunia.
Alisema na kuwataka vijana kabla ya kuamua kufanya biashara lazima uwe na wazo la biashara ili uweze kuwa na uelewa mzuri wa kuifanya biashara hiyo kuliko kufanya biashara bila kuwa na udhoefu nayo.
Waziri Kiruswa aliwataka vijana kuwa wabunifu katika biashara kwani serikalini kuna fursa nyingi za biashara na serikali imetenga mamilioni ya fedha kwa vijana ili waweze kujiajiri na sio vinginevyo.
Alisema Wizara zote zina fursa na unapaswa kujipanga namna ya kuipata fursa hiyo na ndio maana amechukuwa wataalamu kutoka nchini Kenya ili waweze kutoa semina kwa vijana namna ya kuandika wazo na kuifanya biashara hiyo kwa gharama zake binafsi kwa kuwa ana uchungu kuona vijana wenye nguvu wanakaa vijiweni wakisubiri kuomba.
‘’Vijana changamkiani fursa zilizopo serikalini kupitia kongamano hili ili muweze kuwa na uelewa mkubwa wa kufanya biashara kuliko kukopa fedha wakati hujajiandaa kuifanya biashara hiyo’’alisema Kiruswa
Na Wakufunzi wa masuala ya kibiashara kutoka Kenya Dkt John Makokha wa kampuni ya ujasiliamali ya Fayota na Godfrey Mwenda wa Kampuni ya Paysmore Mentor’s waliwaambia vijana kuwa hakuna ajira nzuri kama kujiajiri mwenye na kusema kuwa ajira za serikali ni nzuri ila sio za kutegemea sana.
Walisema wao ni wabobezi katika masuala ya ujasiliamali na wamejiajiri wenye na kuwataka vijana kutumia nafasi ya kongamano hilo kujifunza na hatimaye kupata fursa serikalini kwani serikali ya Tanzania imewajengea wigo mzuri kwa kujikwamua kiuchumi.
Walisema wanafunzi vijana namna bora ya kujiajiri na kuwafunzi namna ya kuandika wazo la kibiashara na iwapo watumia vema mafunzo hayo ana uhakika vijana wa Longido katika muda mfupi ujao wanaweza kuwa matajiri wa kutupowa na wao kuwa walimu wakubwa kwa wengine.
Mmoja wa vijana hao Ikoye Laize na Zainabu Mbilu wamesema kuwa wao ni washiriki wa mara ya pili katika kongamano hilo kwani mwaka jana walishiriki na sasa wanafanya biashara ya kuuza mbuzi na mwingine anauza matunda na mboga mboga na sasa wanajipanga kufanya biashara hiyo nje ya nchi baada ya kuendelea kupata udhoefu kwa kuifanya biashara hiyo.