M23 hawajasitisha mapigano Goma- DRC

CONGO : SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kuwa taarifa kuhusu kusitishwa kwa mapigano yaliyotangazwa na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo ni za uongo.
Msemaji wa Serikali ya Congo,Patrick Muyaya, amesema hakuna kusitishwa kwa mapigano, na badala yake wanachosubiri ni kuondoka kwa waasi hao nchini humo.
Kauli hiyo ya serikali ya Congo inakuja huku Umoja wa Mataifa ukiripoti mapigano makali kati ya M23 na jeshi la Congo. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, alieleza kuwa wamepokea ripoti za mapigano katika Kivu Kusini, lakini hawana taarifa zozote zinazothibitisha kuwa M23 wameikaribia Bukavu.
Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa M23 inapata msaada kutoka kwa kikosi cha wanajeshi 4,000 wa Rwanda. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na mwaka 2012, wakati waasi hao walipouteka mji wa Goma kwa muda na kisha kuondoka baada ya shinikizo la kimataifa.


