Ma-DC Ileje, Mbozi wakabidhiwa magari mapya

SONGWE; Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewakabidhi magari mapya mawili wakuu wa Wilaya za Mbozi na Ileje yaliyonunuliwa na serikali.
RC Chongolo amekabidhi magari hayo leo Jumanne Julai 16, 2024 makao mkuu ya Mkoa wa Songwe yaliyopo Nselewa, Mbozi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Chongolo amesema: “Nashukuru kwa upatikanaji wa vitendea kazi hivi vya wakuu wa wilaya. Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa magari haya.
Soma:Sh bilioni 16 kununua magari 81
“Hizi gari ni imara na wito wangu kwa wakuu wa wilaya yatunzeni magari haya ili yadumu muda mrefu. Wakati wa service ukifika mhakikishe yanafanyiwa yasipitilize muda wake.” amesema Chongolo
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ileje,Farida Mgomi. ambao wamekabidhiwa magari hayo, wameahidi kuyatunza na yatatumika kwa kazi iliyokusudiwa.
“Nashukuru sana Mh Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kunipatia gari muwakilishi wako ili niweze kuwatumikia Wananchi wa Wilaya ya Ileje,”amesema Mgomi.
“Tumesimangwa sana kuhusu haya magari na upande wa pili (upinzani) kuhusu serikali kununua magari haya. Wanahoji magari yananunuliwa ya nini lakini sisi tutawafikiaje wananchi bila kuwa na magari. Tunashukuru Rais Samia kwa kutuletea magari haya,”amesema Mkuu wa Wilaya ya Mbozi.