Maandalizi Kill Marathon yaiva

MOSHI: Maandalizi ya Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2026 yamekamilika, huku jiji la Moshi likijaa washiriki na wageni kutoka nchi mbalimbali.
Tukio litafanyika Jumapili, Machi 22, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), huku Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda akitarajiwa kushiriki kama mgeni rasmi.
Mbio za mwaka huu zitahusisha kilomita 42.1 (Full Marathon), 21.2 (Half Marathon) na 5 za kujifurahisha.
Waandaaji wametoa onyo kwa waendesha pikipiki na baiskeli kuepuka kuwasaidia washiriki ili kuhakikisha ushindani halisi na usalama wa kila mshiriki.
Tukio hili pia linahimiza vijana na wananchi wote kujitokeza, kushiriki kwa furaha huku likiwa na tija katka kuboresha afya, kuimarisha mwili na kuzuia magonjwa yasiyo ya maambukizi.

Mbio za Kilimanjaro Marathon ni fursa ya kipekee ya kuunganisha jamii, burudani na michezo, huku washiriki wakipata faraja ya kipekee ya kuishi mazingira ya mlima Kilimanjaro.
Barabara za Sokoine na Kilimanjaro zitafungwa kwa muda maalum, huku madereva wakishauriwa kutumia njia mbadala za Shanty Town na Rau kuelekea Moshi mjini au Mweka.
Waandaaji wanahimiza kila mshiriki kuzingatia kanuni za usalama, kutumia maji ya kutosha, na kufanya warm-up kabla ya mbio ili kuepuka jeraha.
Mbio hizi zinaendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa, zikionyesha jitihada za serikali, michezo, na utalii katika matukio makubwa yanayovutia washiriki na mashabiki kutoka kila pembe ya dunia.

Tukio la Kilimanjaro Marathon pia limeimarisha historia ya Tanzania kama kitovu cha mashindano ya kimataifa, huku likiendeleza utamaduni wa maisha yenye afya na michezo ya viwango vya juu.



