Mabula awacharukia maafisa ardhi Dodoma

Awataka wafuate wananchi sio kujifungia ofisini

WAZIRI  wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula amewataka maafisa wa sekta ya ardhi nchini kuwafuata na kuwahudumia wananchi katika mitaa yao ili kutoa huduma za ardhi kwa ufanisi.

Akizungumza siku ya leo, 20 Aprili 2023 jijini Dodoma, Dkt Angeline amesema hatua stahiki zitachukuliwa kwa afisa yoyote ambaye hatafuata maagizo hayo.

“Kuanzia wiki ijayo sitaki kukuta watu hapa, fanyeni Cliniki za ardhi kwa muwafuate kwenye mitaa yao wanako husika na mimi ntapita kwenye maeneo hayo halafu nikute hamjaenda ntachukua hatua stahiki kwa sababu kama ni huduma ya kuanzia kwenye maombi mpaka mtu anapata hati kwa nini mrundikane hapa wakati unaweza kuifanya katika mitaa yao huko huko” Amesema Dkt Mabula.

Waziri huyo alilazimika kutoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma zinazotoa huduma za ardhi kwa wananchi na kukuta msongamano mkubwa usiofuata utaratibu na kusababisha kero nyingi kutoka kwa wananchi ambao walimfikishia kero hizo.

Sambamba na hilo amewataka maafisa hao kuongeza muda wa kufanya kazi kuanzia saa mbili kamili asubuhi mpaka saa 12 kamili jioni badala ya muda wa awali ambao walikuwa wanamaliza saa tisa alasiri.

“Kama mikoa mingine wameweza kufanya utaratibu wa kuwafuata wananchi katika mitaa yao kwanini Dodoma isifanyike?, Dar es salaam wanawafuata wananchi mitaani na kuwahudumia, Mwanza wanafanya hivyo hivyo kila siku, Shinyanga wanawafuata wananchi kila siku na hata mkoa wa Mara wanawafuata wananchi kila siku mitaani na kuwahudumia, kwanini sisi hapa Dodoma tupo ofisini tu na kuwasumbua wananchi hapa?,” Alihoji Waziri.

Aidha, alikemea tabia ya umilikishaji wa kiwanja kimoja kwa watu wawili au zaidi unaojulikana kama Double Allocation na kusema maafisa wote wanaohusika na tabia hiyo watachukuliwa hatua.

Habari Zifananazo

Back to top button