WAFANYABIASHARA wadogo (machinga) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Ilala wameanza kuwaondoa wafanyabiashara wanaojiita wajasiriamali wadogo katika Soko la Kariakoo kwa lengo la kukwepa kodi.
Mwenyekiti wa machinga katika Soko la Kariakoo, Stephen Lusinde aliliambia HabariLEO jana kuwa utaratibu wa kuwachuja wamachinga wote katika soko hilo la kimataifa umeanza ili kujua walio halali na wenye sifa ya kuwa machinga.
Alisema kwa wafanyabiashara watakaobainika kutokuwa na sifa ya machinga na waliojipenyeza, watarudishwa walikotoka ili wakalipe kodi stahiki kulingana na biashara yao kwani wanatoa taswira mbaya kwa jamii kuwa machinga wanakwepa kulipa kodi.
Lusinde alikiri kuwapo wafanyabiashara waliojipenyeza katika kundi la wamachinga kwa maslahi ya wafanyabiashara wakubwa na kwamba hata bidhaa wanazouza, wanakosa sifa ya kuitwa wafanyabiashara wadogo kwa sababu thamani yake haiwezi kuwa ya wajasiriamali wadogo.
“Baada ya zoezi hilo kukamilika na kuwatoa wafanyabiashara wote ambao walijipenyeza kinyemela ili wasilipe kodi stahili kulingana na biashara zao, kwa ushirikiano na halmashauri tutaanzisha sheria ndogo za kuwasimamia wamachinga ili kuzuia wasitumike kama kichaka cha kukwepa kodi,” aliongeza Lusinde.
Lusinde ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania, alisema lengo la mchakato huo ni kuwafanya machinga wote walipe kodi stahiki.
Alitoa mfano kuwa kama wamachinga watakuwa na miundombinu bora ya kufanya biashara wataweza kulipa kodi hata kama ni Sh 500 itaisaidia serikali.
Aliongeza kuwa wao viongozi wanataka kuwajenga wamachinga wa sasa na wajao waone ni wajibu wao kulipa kodi.
Kuhusu wamachinga kuondoka barabarani, alisema viongozi wao wamefanya vikao kadhaa na wawakilishi wa serikali kutoka halmashauri na kuwasilisha pendekezo lao la kuwa na eneo mahususi kwa ajili ya wamachinga.
Alibainisha kuwa katika pendekezo lao, wameomba serikali kufikiria kutenga eneo la wamachinga katika mradi mkubwa wa Bonde la Mto Msimbazi ili wamachinga wote wapate kukaa katika sehemu itakayowaepushia jua na mvua.
Aliweka wazi kuwa si kweli kuwa kutokuwepo kwa eneo mahususi kwa ajili ya wamachinga kunahalalisha wao kuziba barabara kwa kupanga bidhaa zao bali kinachotakiwa ni wamachinga kuwa na fikra sahihi kuwa si haki wa busara kupanga vitu barabarani.
Kwa muda mrefu wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakilalamikiwa katika Soko la Kariakoo kuwa wanapanga bidhaa zao barabarani na kuleta usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara hizo.