Madaktari: Mabadiliko tabianchi yanaongeza magonjwa

MADAKTARI na watalaamu wa mazingira wamesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakichangia ongezeko la magonjwa ya moyo na saratani. Wataalamu hao walisema ongezeko la joto, ukame na uchafuzi wa hewa na mazingira vinachangia ongezeko la magonjwa ya sugu ya mfumo wa hewa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge alisema kukiwa na ukame, wanawake wanaopata ujauzito hawapati lishe inayohitajika yakiwamo madini ya folic yanayopatikana katika mboga na matunda, hivyo watoto wanaweza kuzaliwa wakiwa na matundu kwenye moyo.

“Lakini pia kutokupata hewa ambayo ni safi inaweza kuchangia magonjwa ya moyo, mapafu,”alisema Dk Kisenge.

Alisema wagonjwa wa shinikizo la damu wanapopata joto kali, hupata msongo wa mawazo hivyo kusababisha moyo kwenda mbio, kuchoka na kusababisha kiharusi.

Dk Kisenge alishauri wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya wabaini mapema kama wana matatizo na wazingatie lishe bora, wafanye mazoezi.

Asema uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliokithiri ni hatari. Daktari bingwa wa magonjwa ya kisukari, Prof Andrew Swai alisema kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, mazingira yanabadilika, mfumo wa maisha unabadilika na aina ya vyakula pia vinabadilika.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa, Fransis Furia alisema muunganiko wa wanyama na watu vinasaidia kupunguza baadhi ya magonjwa.

Profesa Furia alisema zamani ilikuwa inaaminika kuwa magonjwa kama pumu na mzio yalikuwa hayatokei vijijini kwa sababu wanacheza kwenye matope,wanakutana na minyoo na wadudu kwenye udongo.

“Sasa hivi kwa sababu ya mabadiliko, mvua hazinyeshi na wadudu wanakufa kwa hiyo hatukutani nao, sasa hivi tunajenga nyumba, tunaweka marumaru, hawataki watoto kupata udongo tunataka wacheze huko wakutane na wadudu na wawazoee,”alisema.

Profesa Furia alisema uchafuzi wa hali ya hewa unachangiwa pia na moshi ukiwamo wa sigara wenye madhara kwa watu ambao wako karibu na watumiaji.

Mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira, Richard Mayungi alisema mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuchangia magonjwa yasiyoambukiza kwa kubadili mfumo wa maisha ya binadamu.

Mayungi alisema kama mwili wa binadamu umezoea nyuzi joto 24 halafu hali ikabadilika kuwa nyuzi joto 28, lazima mfumo utahitaji maji mengi na upumuaji unabadilika.

Habari Zifananazo

Back to top button