KATIBU Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati Dodoma, Jasmini Awadhi, amewataka wakuu wapya wa wilaya walioteuliwa kuheshimu na kuviishi viapo vyao walivyoviapa kwa uadilifu na uaminifu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Mkuu wa wilaya ya Chemba, Gelard Lomward Mongela katika hafla fupi iliyofanyika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Januari 30, 2023.
“Hakikisheni mnajitoa kutumikia viapo mlivyotoa mbele yetu na kuviweka katika kumbukumbu zenu za kila siku, ili viwasidie kuyakunbuka yale yote yaliyoelezwa katika viapo hivyo mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku,” alisema.
Pia alimpongeza mkuu mpya wa wilaya ya Bahi, Godwin Gondwe na Mkuu wa Wilaya Mpwapwa, Sophia Kizigo waliohamishiwa mkoani Dodoma katika mabadiliko ya vituo vya wakuu wa wilaya yaliyofanyika hivi karibuni.
Hafla ya kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya Chemba na kuwakaribisha wakuu wa wilaya wapya, ilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyemule, ambayo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma, Viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na menejimenti ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.