MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, amezindua ‘App’ mpya ya kuwawezesha madereva kupata huduma za mafuta kwa urahisi nchini Tanzania.
Huduma hiyo iliyopewa jina la Wese, itawawezesha madereva kupata fursa ya kununua mafuta na kulipa baadaye, bila riba wala kamisheni.
Akizungumza jijini Dar es Salam leo Oktoba 26, 2022 Gondwe amesema, Wese ni jukwaa la kifedha na biashara linalounganisha kwa pamoja sekta ya uchukuzi, petroli na fedha.
Amesema huduma hiyo inatarajiwa kufanyiwa majaribio jijini Dar es Salaam mwezi ujao, ikilenga kuwawezesha madereva wote wa magari makubwa, madogo, daladala, pikipiki na bajaji na wafanyabiashara kupata huduma ya mafuta kwa unafuu zaidi.
Gondwe amesema kuzinduliwa kwa ‘App’ hiyo ni fursa kwa vijana hususani boda boda na bajaji.
“Mfumo wa kieletroniki utaenda kubadili maisha ya vijana, itawajengea nidhamu ya kutunza fedha na kukua kibiashara,” amesema.
Naye mwanzilishi wa mfumo huo wa Wese, Francis Ekeng ambaye ni raia wa Nigeria, akizungumzia mfumo huo amesema unafanana na mfumo kama wa taxi mtandao, ambao muhusika atalazimika kupakua ‘app’ hiyo kwenye simu yake ya kiganjani na kujisajili.
“Mtu akishajisaji atakuwa na uwezo wa kujaza mafuta ya gharama yoyote anayotaka katika kituo chochote cha mafuta nchi nzima, ila atatakiwa kulipa kabla ya saa sita usiku,” amesema.
Akifafanua zaidi anasema iwapo dereva atashindwa kulipa deni kwa wakati, atapigwa faini na iwapo atalipa kwa wakati atapata fursa ya kukidhi vigezo vya kukopesheka zaidi kutokana na uaminifu.
“Kila dereva anapochukua mafuta na kulipa bila kupata adhabu au kushindwa, pointi inatolewa ambayo inamjengea sifa yake ya kukopesheka zaidi,” amesema.