TANGA: TUME ya Madini imewataka watumishi wake nchini kutumia muda mwingi kufanya kazi, huku wakitenga muda wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali ili kuimarisha afya ya mwili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza leo Juni 14, 2024 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Ramadhan Lwamo amesema siku zote afya ndio kazi , afya mgogoro hakuna kazi.
Mhandisi Lwamo amesema hayo akifunga bonanza la wakurugenzi, mameneja kutoka Tume ya Madini Makao Makuu Dodoma na maofisa madini wakazi wa mikoa lililofanyika kwenye viwanja vya Mnyanjani jijini Tanga.
‘Michezo ni furaha, inaimarisha uhusiano na kuboresha afya zetu watumishi, baada ya bonanza ‘reflection’ yake tunaiona kwenye matokeo ya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya serikali,”amesema Lwamo.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tume CPA William Mtinya akizungumza amesema, Tume imeweka utaratibu wa kuhamasisha watumishi wake kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali, ili kuwaweka vyema kiafya na kuwa imara katika utendaji kazi wao.
Amesema pia Tume inatekeleza maagizo ya Serikali kwamba kila taasisi idumishe michezo ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yamekuwa yakisumbua jamii na kwamba bonanza hilo pia huleta mshikamano wa wafanyakazi na kubadilishana mawazo.
“Tumekutana kujadili mikakati ya kukusanya maduhuli ya serikali, kuimarisha afya zetu na maofisa madini wakazi wa mikoa,”amesema CPA Mtinya.
Naye Ofisa Madini Mkazi wa Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu akizungumzia matokeo ya kufungwa mabao 2-0, amesema kuwa wamekubali matokeo, walizidiwa na mchezo.
Katika Bonanza hilo timu ya soka ya Tume ya Madini kutoka Makao Makuu Dodoma iliibugiza RMO’s mabao 2-0 katika mchezo wa fainali na kutwaa Kombe.
Katika bonanza hilo vikombe na medali zimetolewa kwa washindi ikiwa ni pamoja na Mfungaji Bora mpira wa miguu Azihar Kashakara kutoka Tume Makao Makuu, Kipa Bora CPA Wiliam Mtinya kutoka Tume Makao Makuu na Mchezaji Bora Mhandisi Sabai Nyansiri kutoka Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Singida.
Licha ya mpira wa miguu pia bonanza hilo limehusisha michezo ya kuvuta kamba, kukimbia mita 100 na kufukuza kuku.