Timu za TPA zatwaa ubingwa SHIMMUTA

MOROGORO: TIMU za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) zimehitimisha Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA) 2026 kwa mafanikio katika mchezo wa kuvutana kwa kamba, baada ya timu zake za wanawake na wanaume kutwaa ubingwa na wachezaji wake wawili kuzoa tuzo za wachezaji bora.
Katika mashindano hayo yaliyoanza Novemba 6 na kuhitimishwa leo, Novemba 21, mwaka huu mkoani Morogoro, TPA imeibuka mshindi wa fainali zote mbili za mchezo wa kuvutana kwa kamba, licha ya kushindwa kutwaa ubingwa wa jumla kwa tofauti ya alama mbili.
Kwa upande wa wanawake, TPA iliifunga Tume ya Madini (MC) kwa mivuto miwili kwa bila, ikitumia sekunde sita katika mvuto wa kwanza na sekunde tano katika mvuto wa pili.

Kwa upande wa wanaume, timu hiyo iliibuka na ushindi wa mivuto miwili kwa bila dhidi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ikitumia sekunde tisa katika mvuto wa kwanza na sekunde nane katika mvuto wa pili.
Mbali na ushindi huo, wanamichezo wawili wa TPA walitunukiwa tuzo za wachezaji bora, ambapo Ashura Msisi alitangazwa kuwa Mchezaji Bora kwa upande wa wanawake, huku Mathias Lyon akitwaa tuzo hiyo kwa upande wa wanaume.
Katika matokeo ya jumla, TPA ilikusanya alama 14 na kushika nafasi ya pili, huku Mzinga ikiibuka bingwa kwa kupata alama 16.

Hata hivyo, safari ya TPA katika mashindano hayo imekuwa na matokeo tofauti katika michezo mbalimbali, baada ya kushindwa kutetea baadhi ya mataji iliyokuwa ikiyashikilia kwa miaka kadhaa.
Katika mchezo wa netiboli, TPA imeshindwa kutetea ubingwa wake baada ya kutwaa mataji mara tano mfululizo.
Hali hiyo pia imejitokeza katika mpira wa kikapu kwa upande wa wanaume, ambapo timu hiyo iliyokuwa imetwaa ubingwa mara tano mfululizo imemaliza mashindano ya mwaka huu katika nafasi ya tatu.
Katika mchezo wa mpira wa wavu, timu ya wanaume ya TPA imeshika nafasi ya pili, huku wanawake wakimaliza katika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa soka, TPA imemaliza katika nafasi ya tatu, wakati katika riadha imepata nafasi ya pili baada ya wanamichezo wake kutwaa jumla ya medali tisa, zikiwemo tatu za dhahabu, tatu za fedha na tatu za shaba.
Matokeo hayo yanaonesha mwenendo wa TPA katika mashindano ya mwaka huu, huku ushindi katika kuvutana kwa kamba na mafanikio katika riadha ukiwa sehemu ya matokeo yaliyopatikana licha ya kupoteza baadhi ya mataji.
Mashindano hayo yamehitimishwa na kufungwa rasmi na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Pius Chaya.



