Zaidi ya 700 waungana kupigania afya bora

DAR ES SALAAM: WAKATI magonjwa yasiyoambukiza yakiendelea kuwa changamoto inayohitaji uelewa na hatua za kinga, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeelekeza nguvu katika kuhamasisha jamii kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora na kufuatilia afya zao.
Kupitia matembezi na mbio za hisani zilizofanyika Novemba 21, 2026, katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam, MUHAS kimewakutanisha washiriki zaidi ya 700, wakiwemo wanafunzi, wahitimu, wafanyakazi na wadau wa afya kutoka ndani na nje ya nchi.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuijengea jamii utamaduni wa kujali afya na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kupitia mabadiliko ya maisha ya kila siku.
Akizungumza katika tukio hilo, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesema Serikali imekuwa ikihimiza wananchi kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha afya na kuzuia magonjwa.

Amepongeza MUHAS kwa kuandaa matembezi hayo, akisema yamekuwa fursa ya kuwakutanisha watu mbalimbali wenye uhusiano na chuo hicho, wakiwemo waliowahi kusoma na kufanya kazi hapo.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema matembezi hayo yamefikia msimu wa tano tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa kujikinga na magonjwa kupitia mtindo bora wa maisha.

Amesema ushiriki wa mwaka huu umehusisha pia wadau kutoka Marekani, Sweden na Ujerumani, akiahidi kuwa chuo kitaendeleza programu hiyo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Baadhi ya washiriki wamesema programu hiyo imekuwa chachu ya kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli za kimwili na kujenga mazoea ya kujali afya zao.

Katika tukio hilo, washiriki walishindana katika umbali wa kilomita moja, tano, 10 na 15, huku washindi wa kila kundi wakikabidhiwa vyeti na mgeni rasmi.



