Madiwani waidhinisha Kishoa akatwe mshahara

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Kibaha limeidhinisha kukatwa asilimia 15 ya mshahara kwa kipindi cha miaka mitatu Mhandisi wa halmashauri hiyo kwa kushindwa kusimamia mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi.
Akitoa maazimio ya kikao hicho cha baraza la madiwani cha robo mwaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Musa Ndomba amesema kuwa mtumishi huyo alisababisha mradi huo kuwa na gharama kubwa.
Ndomba amesema kuwa uamuzi huo ni hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na baraza kwa Mhandisi huyo wa Halmashauri hiyo ambaye hakufuata utaratibu wa manunuzi (BOQ) ya ujenzi wa nyumba hiyo.
“Kutokana na kutofuata taratibu za manunuzi kulitokea changamoto kwenye ununuzi wa vifaa kwani haukufuata bajeti iliyopangwa hivyo gharama za ujenzi kuwa kubwa,” ameeleza Ndomba.
Amesema baada ya changamoto hiyo kutokea ilibainika kuwa katika usimamizi wa miradi ilionekana kuna maeneo kafanya uzembe hivyo baraza la madiwani na kamati ya fedha ziliamua kumchukulia hatua za kinidhamu.
“Taratibu zote zimefuatwa kwa kamati za uchunguzi na kufanya kazi yake na zikapendekeza adhabu hiyo na hilo litakuwa fundisho kwa watumishi wengine kwa kutakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazowaongoza,” alisema Ndomba.
Aidha alisema kuwa anawakata watumishi wote kuanzia Halmashauri hadi kwenye Mtaa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na wasipingane na miongozo ya kazi zao kwani miradi ya maendeleo itakuwa haina tija na kurudisha nyuma utoaji huduma kwa wananchi.