Magereza washauri malezi bora watoto wa kiume

JESHI la Magereza limewashauri wazazi kuanza kubadilisha mwelekeo wa makuzi na malezi kwa kuweka nguvu kubwa kuwalinda watoto wa kiume ili wawe shupavu .

Kamishna wa Jeshi la Magereza anayesimamia Kamisheni ya Sheria na Uendeshaji, Nicodemus Tenga ametoa rai hiyo kwenye mahafali ya 64 ya Shule ya Sekondari Mzumbe ya wavulana wenye vipaji maalumu iliyopo Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Tenga alimwakilisha Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Jeremiah Katungu kwenye mahafali hayo ambapo jumla ya  wahitimu1 16 watarajiwa kufanya mitihani yao ya  kidato cha nne Novemba mwaka huu.

Advertisement

Amesema jitihada kubwa zimefanyika na zinaendelea kufanyika kwenye jamii ya kuendeleza  kampeni kubwa zaidi ya kuwalinda watoto wa kike ,lakini kwa watoto wakiume wakiwa wameachwa nyuma.

“Jamii imepinga kampeni kubwa sana kuwalinda watoto wakike lakini kwa watoto wakiume wameachwa…sasa wazazi muda ndiyo huu ninawaombeni tuacheni na yale tufanye shime kuwalinda watoto wakiume ili waje kuwa kina baba,”

“…kwa namna hii mzazi mwingine anakuja kuilaumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , je hapo kuna lawama ya serikali,” amehoji Tenga.

Hivyo ameendelea kutoa rai kwa wazazi kutumiza wajibu wao katika kutengeneza familia imara, watoto imara, kizazi cha kesho imara na taifa lijalo imara.

Pamoja na hayo ameipingeza  shule hiyo ya serikali kwa kufanya vizuri katika mitihani ya taifa ya kidato cha nne pamoja na kidato cha sita ikiwa na kuwajengea wanafunzi stadi za ujuzi na ubunifu ambazo ni chachu cha wao kuendeleza vipawa vyao vitakavyowapa fursa ya kujitengemea siku za usoni.

Tenga aliipongeza shule na bodi yake kutokana na juhudi zinazochukuliwa za kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ,ambapo katika kuunga mkono, kwa niaba ya jeshi hilo alichangia Sh milioni 1 kusaidia uboreshaji miundombinu ya shule hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo, Mbaraka Kupela amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali  katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa maji na uchakavu wa nyumba za walimu.

“ Kwa sasa tunatengemea maji yanayotolewa kutoka Chuo Kikuu Mzumbe  lakini hayatoshereji  kukidhi mahitaji ya shule mzima,” amesema  Kupela.

Mkuu wa shule aliitaja changamoto nyingine ni  uchakavu wa nyumba za watumishi na hivyo kuwa hatarishi zaidi hasa nyakati za  mvua na kutishia usalama kwa walimu na familia zao.

Amesema katika kutatua changamoto hizo, wazazi, uongozi wa shule pamoja na bodi ya shule wameafikiana kila mzazi mwenye mwanafunzi aweze kuchangia  Sh 100,000.

Amesema pia waliowahi kusoma katika shule hiyo wameazisha umoja  wao  na kuchangia Sh milioni 180 ambazo zimetumika kukarabati vyoo vya wanafunzi.

Pia kiasi kingine cha Sh milioni 30 zimetumika ununuzi wa vitabu muhimu wa kitaaluma kwa wanafunzi kuwekwa katika maktaba ya shule.

Mkuu wa shule hiyo amasema mwaka 1992 iliteuliwa kuwa shule maalumu ya vipaji maalum ikipokea wanafunzi wenye ufauli mkubwa wa darasa la saba na kidato cha nne  ambapo ina uwezo wa kupokea wanafunzi 720 kuanzia  kidato cha kwanza hadi cha sita.

Amesema lakini kwa sasa ina idadi ya wanafunzi 789 kati yao wa kidato cha kwanza hadi cha nne ni 471 na wa kidato cha tano hadi sita kidato ni 318.