Mageuzi yaja sekta ya uvuvi kukuza uchumi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi utasaidia kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka kutoka asilimia 1.8 ya sasa.

Majaliwa amesema mpango huo utakaotekelezwa kwa miaka 15 kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037, ni muhimu katika ukuaji wa sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu.

Waziri Mkuu alisema hayo Jumanne Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam (UDSM).

Aliwaeleza wadau wa sekta ya uvuvi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ina nia ya dhati kuhakikisha kila mmoja ananufaika na sekta hiyo.

“Tutaendelea kupokea mapendekezo yenu ili tuweze kuboresha sekta hii, ubunifu wenu ni muhimu, wote tunataka tuzungumze lugha moja,” alisema Majaliwa.

Alisema mpango huo unaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mapinduzi kwenye sekta zote ikiwamo sekta za uzalishaji.

“Mpango huu utasaidia kwa kiwango kikubwa kutekeleza dhamira hiyo njema ya Mheshimiwa Rais, tunataka twende kwa kasi zaidi,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema uwepo wa mipango katika sekta ya uvuvi utawezesha rasilimali hiyo kulindwa, kusimamiwa, kuendelezwa, kuhifadhiwa na kutumiwa kwa njia endelevu na hatimaye kuchangia kikamilifu katika kutoa ajira, kipato, chakula na lishe kwa jamii ya Watanzania.

Alisema utekelezaji wa mpango huo utakuwa chachu ya kuendeleza kasi ya ukuaji wa sekta ya uvuvi na utasaidia kuongeza kiasi cha samaki na mazao ya uvuvi yaliyochakatwa na kusafirishwa nje ya nchi kwa asilimia 30.

“Mpango huu utakuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi kutoka tani 473,592 hadi kufikia tani 639,092, sawa na ongezeko la asilimia 35,” alisema Majaliwa.

Aliziagiza wizara na taasisi za serikali, mamlaka za serikali za mitaa, sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali, madhehebu ya dini na wadau wa maendeleo kuupokea.

“Uzingatieni mpango huu katika mipango yenu ya kisekta na kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kufanikisha utekelezaji wake kwa maslahi mapana ya Taifa,” aliongeza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema mpango huo utakuwa jumuishi na hautamuacha yeyote anayejishughulisha na sekta ya uvuvi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uvuvi Tanzania, Profesa Yunus Mgaya alisema mpango huo utaleta maendeleo katika sekta ya uvuvi kwa kipindi cha miaka 15.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Tipo Nyabenyi alisema wamefurahi kushirikishwa na serikali katika uandaaji wa mpango huo ambao wanaamini kwa kiasi kikubwa utaleta mchango katika kutatua changamoto mbalimbali za sekta hiyo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button