Mahakama Kuu Kanda ya Iringa yatangaza maadhimisho ya miaka 20

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imeanza rasmi kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, ikiwa imejikita kuonesha safari yake ya mabadiliko, mafanikio, changamoto na mwelekeo wake wa utoaji haki nchini.

Kupitia kaulimbiu “Safari ya Miaka 20 ya Mahakama Kuu: Tulikotoka, Tulipo na Tunakoelekea,” mahakama hiyo inatarajia kuwakutanisha wananchi na wadau wa sheria katika majadiliano, elimu na shughuli mbalimbali zinazolenga kuongeza ufahamu wa umma juu ya mifumo ya utoaji haki.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa leo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dunstan Ndunguru, alifafanua kuwa maandalizi yote ya maadhimisho hayo yapo katika hatua ya mwisho, huku akisisitiza kwamba maadhimisho ya mwaka huu yamejengwa kwa dhana ya “mahakama ya wananchi.”

Jaji Ndunguru alisema kuwa siku ilipoanzishwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa mwaka 2005, dhamira kubwa ilikuwa ni kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi ambao hapo awali walilazimika kusafiri hadi Dodoma, Mbeya, Songea au Dar es Salaam kufuata huduma za Mahakama Kuu.

“Leo tunapotimiza miaka 20, tumepata nafasi ya kutazama nyuma kuona tulipotoka, kutathmini tulipo, na kujiuliza tunakoelekea. Safari hii ni ya wananchi wote—wale tuliowahudumia na wale wanaoendelea kuitumia Mahakama kama sehemu salama ya kupata haki,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Ndunguru, Mahakama Kuu Iringa inakuwa miongoni mwa kanda za mwanzo nchini kufanya maadhimisho haya kwa namna ya kitaifa, hatua ambayo inaonesha dhamira ya mahakama hiyo kupanua uwazi, ushirikishwaji na elimu kwa wananchi.

Katika ufafanuzi wake, Jaji Ndunguru alieleza jinsi miaka 20 ya Mahakama Kuu Iringa ilivyokuwa chachu ya mageuzi makubwa yanayoonekana leo.

Alisema mahakama imefanikiwa kujenga na kukarabati majengo, kuongeza idadi ya watumishi, kuboresha vyumba vya kusikilizia mashauri na kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi na wananchi.

Lakini mafanikio makubwa zaidi, kwa mujibu wake, yameonekana katika maendeleo ya TEHAMA ambayo yamebadilisha mfumo mzima wa utoaji haki nchini.

“Teknolojia imeleta mageuzi. Mfumo wa eCMS, Video Conference kwa mahabusu, na upatikanaji wa taarifa kwa njia ya mtandao vimeharakisha utoaji haki na kuongeza usalama. Haya ni mageuzi tuliyoyapigania kwa miaka mingi, na leo hatua zake zinaonekana,” alisema.

Katika safari ya miaka 20, moja ya changamoto kuu ilikuwa ni mlundikano wa mashauri. Hata hivyo alisema, kupitia mikakati ya kitaifa na kikanda, kampeni za kusafisha mashauri ya muda mrefu, pamoja na uhimilishaji wa usuluhishi (ADR), Mahakama Kuu Iringa imepunguza kwa kiasi kikubwa mashauri yaliyokwama na kuongeza kasi ya utoaji maamuzi.

Mahakama pia imeongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za kisheria, jambo ambalo limesaidia kupunguza migogoro isiyolazimu kufika mahakamani.

Pamoja na mafanikio makubwa ya miaka 20, changamoto kadhaa zimeendelea kujitokeza akitaja mojawapo kuwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu matumizi ya TEHAMA katika kufungua na kufuatilia mashauri.

“Wananchi pia bado wanahitaji elimu zaidi kuhusu taratibu za mahakama, umuhimu wa usuluhishi, na mbinu sahihi za kutafuta haki bila migogoro,” alisema.
Aidha alisema, mahakama inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha makundi maalumu—wanawake, watoto na watu wenye ulemavu—wanapata huduma za haki bila vikwazo vyovyote.

Alisema kuelekea siku ya kilele tarehe 15 Desemba 2025, Mahakama Kuu Iringa imeandaa wiki ya elimu kwa wananchi kupitia vipindi vya redio na televisheni.

Vipindi hivyo vitatoa elimu kuhusu taratibu za mirathi, uandishi wa wosia, kuasili watoto na taratibu zake, sheria za ukatili wa kijinsia, uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, haki za watoto, na utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Alisema Desemba 12, kutafanyika mdahalo mkubwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), utakaowakutanisha wanazuoni, watumishi wa mahakama na wadau wa sheria kujadili mifumo ya kisasa ya utoaji haki.

Desemba 13 alisema, kutakuwa na matembezi ya maadhimisho, yakilenga kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kutii sheria na kutumia njia sahihi za kutatua migogoro.

Kwa upande wa wananchi, Mahakama Kuu Iringa imewahimiza kujitokeza kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zinazotarajiwa kufanyika, hususan vipindi vya elimu na matembezi ya maadhimisho, ili kuongeza uelewa kuhusu mfumo wa haki na nafasi yao katika kuimarisha amani na ustawi wa jamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button