Mahakama yaahirisha uamuzi kesi ya Lissu

DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi kuhusu kesi ya kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, Mei 6, mwaka huu.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza majibu ya pingamizi yaliyotolewa na upande wa Jamhuri kuhusu uamuzi wa kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao au mshitakiwa kupelekwa mahakamani.
Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini huku upande wa jamhuri ukiwa na mawakili wanne.
Jamhuri iliongozwa na wakili wa serikali mwandamizi, Job Mrema na upande wa utetezi ukiwa na mawakili 31 wakiongozwa na Wakili Mpare Mpoki.
Kesi hiyo iliyosikilizwa kwa njia ya mtandao ilianza kwa upande wa jamhuri kujibu hoja pingamizi zilizotolewa na utetezi juu ya kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandao.
Awali, Jeshi la Magereza walipoulizwa kuhusu uwepo wa mshitakiwa walidai kuwa Lissu aligoma kufika katika chumba maalumu cha kusikilizia kesi hiyo kwa njia ya mtandao.
Mrema alianza kwa kutoa majibu ya pingamizi la kwanza lililotolewa na upande wa utetezi la kupinga ahirisho la siku 30 lililotolewa na upande wa jamhuri.
Alidai kuwa hoja ya kuahirishwa kwa kesi hiyo kwa siku 30 inatokana na kifungu cha 225 kifungu kidogo cha pili cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Mrema alidai kifungu hicho kinatoa ukomo wa muda wa mahakama kuahirisha kesi endapo mshitakiwa atakuwa nje kwa dhamana kama ilivyo kwa Lissu baada ya Aprili 10, kupewa dhamana licha ya kushindwa kutoka kutokana na kuwa na shitaka lingine la kesi ya uhaini.
Alidai kuwa upande wa utetezi walishindwa kuonesha ni sheria ipi inayoonesha kuwa kesi hiyo haiwezi kuahirishwa kwa muda huo na kuomba mahakama itambue kifungu tajwa na kusikiliza ombi la upande wa Jamhuri.
Katika hoja nyingine waliyotolea majibu upande wa jamhuri ni kuhusu utetezi kuwasilisha pingamizi kuwa walizuiwa na Jeshi la Magereza na Polisi kuonana na mteja wao (Lissu) akiwa mahabusu Ukonga.
Mrema alidai Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza pingamizi hilo kwa sababu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi zinahusiana na tuhuma dhidi ya watumishi wa umma (Magereza, Jeshi la Polisi na ‘Maofisa wengine’).
Mrema alidai kama upande wa utetezi wanatuhuma dhidi ya watumishi wa Magereza na Jeshi la Polisi walipaswa kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia sheria.
Pia, alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza hoja zinazohusu mapitio ya sheria kama zilivyowasilishwa na upande wa utetezi.
Mrema alidai upande wa utetezi haukufuata sheria na kanuni zilizowekwa na Jeshi la Magereza za kuwasiliana na mahabusu au wafungwa kwa njia ya barua.
Alidai upande wa Jamhuri uliwasiliana na Jeshi la Magereza kufahamu kama mawakili wa Lissu waliwasilisha barua na walibaini kuwa hakukuwa na barua yoyote kutoka kwa mawakili hao kwenda kwa Magereza.
Aidha, pingamizi mojawapo lilikuwa kuhusu upande wa utetezi kudai kesi hiyo iendeshwe mbele ya mahakama ya wazi na kila mtu apate nafasi ya kuifuatilia sio kupitia mtandao kama ilivyofanyika.
Mrema alidai sheria imezungumza kuwa mshitakiwa ana haki ya kusomewa mashitaka ya awali katika ya Mahakama ya Wazi kukiwa na mshitakiwa, hakimu, wakili wa serikali na wakili wa utetezi.
Alisema usikilizaji wa shauri hilo kupitia njia ya mtandao unawezekana kama mshitakiwa, mawakili na hakimu anayesikiliza kesi hiyo wote watakuwepo na kwamba sheria inayoelezea kuwa mahakama ya wazi inaweza kusikiliza kesi hata kwa njia ya mtandao kama ilivyofanyika.
Alidai kuwa upande wa utetezi ulichanganya juu ya maana na tafsiri ya mahakama ya wazi na mahakama ya mtandao.
Mrema alidai upande wa utetezi unaonesha kuwa njia ya mtandao sio mahakama ya wazi hivyo hiyo ni tafsiri potofu na kuiomba mahakama kutupilia mbali hoja hiyo.
Alidai kuwa shauri hilo kusikilizwa kwa mtandao sio kificho ni namna ya usikilizwaji wake.
Mrema alisisitiza kuwa utaratibu wa mashauri yanayoendeshwa kwa njia ya mtandao huwa na kanuni zinazoonesha kuwa mahakama inaweka wazi namna ya kuwasilisha nyaraka kwa pande zote kupitia mfumo mahakama wa ‘Judiciary Management System’.
Alidai uamuzi wa kuendesha shauri hilo kwa njia mtandao haujaathiri amri iliyotolewa Aprili 10, 2025 kwa mujibu wa kanuni ya 4 (6) ya 2021.
Hii ni baada ya upande wa utetezi kudai kuwa amri ya mahakama imekiukwa baada mahakama kusikiliza shauri hilo kwa njia ya mtandao na sio kama iliyotarajiwa.
Mrema alidai, “Uamuzi uliotolewa Aprili 10, 2025 ulilitaka shauri hilo kuanza kusikilizwa hoja za awali Aprili 24, na ndivyo ilivyokuwa lakini upande wa utetezi waliweka pingamizi na mshitakiwa kutoenda katika chumba cha kusomewa mashitaka yake kwa njia ya mtandao”.
Aliongeza: “Aprili 10, 2025 mahakama haikutamka itasikiliza shauri kwa njia gani hivyo kilichofanywa ni utaratibu wa kawaida wa mahakama hiyo”.
Mrema alidai amri iliyotolewa Aprili 10, ni mshitakiwa kupelekwa mahabusu na ni jukumu la magereza kumpeleka mahabusu wanayoiona inafaa na kwa wakati sahihi.
Aliomba mahakama ihairishe shauri kwa siku 30 ili upande wa utetezi wamshawishi mshitakiwa kusomewa hoja za awali kupitia mtandao.