MAHAKAMA ya Juu nchini Kenya imethibitisha ushindi wa Dk William Ruto kuwa Rais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, mwaka huu.
Mahakama hiyo imesema malalamiko yote tisa yaliyoletwa na upande wa walalamikaji hayakuwa na ushahidi wa msingi kuthibitisha madai yao.
Jaji Mkuu wa Kenya, Martha Koome alitoa uamuzi huo wa mahakama hiyo jana jijini Nairobi, akithibitisha kuwa mlalamikiwa Dk Ruto alifanikiwa kufikia takwa la Katiba la kupata asilimia 50 jumlisha na kura moja.
Jaji Mkuu Koome alisema kesi iliyowasilishwa na Mgombea Urais kwa tiketi ya Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ilikosa ushahidi wa kutosha wa kuishawishi mahakama kuamini madai yake na badala yake madai hayo yalijaa uvumi na porojo.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa 1:30, Jaji Mkuu Koome alipangua hoja zote tisa zilizoletwa mahakamani na walalamikaji kama kigezo cha kuonesha kuwa ushindi wa Dk Ruto haukuwa halali na kuiomba mahakama itengue ushindi huo.
Alisema mahakama imekataa madai ya walalamikaji kwamba tume ilihesabu mpaka kura zilizokataliwa hali iliyompa ushindi Naibu Rais huyo kwa sababu kura hizo haziwezi kujumlishwa katika hesabu ya kumtafuta mshindi na kuongeza kuwa mbinu iliyotumiwa na Tume ya Uchaguzi kupata asilimia 64.4 ya wapiga kura ilikuwa sahihi.
Kuhusu ni nani aliyekuwa na uwezo wa kujumlisha na kuthibitisha matokeo katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), Koome alisema mamlaka ya kujumlisha na kuthibitisha matokeo ya uchaguzi wa urais hayatokani na mwenyekiti, bali tume.
Alisema makamishna wanne waliojitenga na kutoa taarifa kwa wanahabari hawakutoa hati yoyote inayoonesha matokeo yalibadilishwa na hawakueleza ni kwa nini walishiriki katika mchakato wa uhakiki ambao wanasema haukuwa wazi.
Aidha, alisema madai ya kuingiliwa kwa mfumo wa teknolojia wa IEBC hayakuthibitishwa kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuonesha mfumo huo katika tovuti ya IEBC uliingiliwa na yeyote ili kuvuruga matokeo.
Aliongeza kuwa tume ilieleza vya kutosha jinsi mfumo ulivyopokea fomu za matokeo zilizowekwa katika tovuti yake na kwamba zote zilikuwa sawa na zile zilizowasilishwa katika kituo kikuu cha kuhesabia kura.
“Majaji hawakushawishiwa na madai kwamba teknolojia iliyotumiwa na IEBC ilifeli katika uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi kiasi cha kuathiri matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa IEBC,” alisema Jaji Mkuu Koome.
Aliwakosoa mawakili wa Odinga kwa kutoa madai ambayo hayana ushahidi pamoja na mawakili waliowasilisha ushahidi wa kupotosha, akisema vitendo hivyo havistahili mahakamani.
Baada ya hukumu hiyo, Rais Mteule Dk Ruto aliyakaribisha maamuzi hayo akisema Kenya imethibitisha kuwa kisiwa cha demokrasia Afrika na kuahidi kuimarisha demokrasia katika utawala wake.
Aliwashukuru Wakenya kwa kuchagua muungano wake huku akisema shujaa wa uchaguzi huo ni Wafula Chebukati ambaye ni Mwenyekiti wa IEBC na shujaa wa sheria na haki ni Mahakama ya Kenya.
Alisema serikali yake itaanzia pale walipoishia akiwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa kutekeleza yale yote waliyowaahidi wananchi wa Kenya. Alimshukuru mshindani wake, Raila na kuahidi kufanya naye kazi.
Raila ambaye huo ni Uchaguzi Mkuu wake wa tano kuwania urais na kushindwa, mbali na kukubaliana na hukumu hiyo, alisema juhudi zake zitaendelea kuhakikisha demokrasia ya Kenya inazidi kuimarika.
Taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na Raila, ilisema licha ya kwamba waliwasilisha hoja na ushahidi wa kutosha, hawana budi kukubali uamuzi wa mahakama kwa kuwa ndio sehemu ya mwisho ya utoaji wa haki.
Kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi duniani ilikuwa na hoja tisa ikiwamo iwapo teknolojia iliyotumiwa na IEBC ilifikia viwango vya ubora na kuwezesha uchaguzi unaoweza kuthibitishwa kuwa salama kwa lengo la kutoa matokeo sahihi na yanayoweza kuthibitishwa.
Hoja nyingine ni iwapo kulikuwa na aina yoyote ya kuingilia jinsi fomu 34A zilivyopakuliwa na kuwasilishwa kwenye tovuti ya IEBC, iwapo kulikuwa na tofauti kati ya fomu 34A zilizopakuliwa katika tovuti ya IEBC na kuwasilishwa katika kituo cha kujumlisha kura na walizopewa mawakala katika vituo vya kupiga kura.
Vilevile iwapo kuahirishwa kwa uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Kakamega na Mombasa na maeneo ya Bunge manne kulichangia kupunguza idadi ya wapiga kura waliojitokeza kupiga kura na kuathiri kura za mlalamikaji ambaye ni Raila.
Pia iwapo kulikuwa na tofauti isiyoeleweka kati ya kura za urais na za nyadhifa nyingine, iwapo IEBC ilijumlisha na kuthibitisha kwa mujibu wa sheria, iwapo Rais Mteule Ruto alipata asilimia 50+1 ya kura zote zilizopigwa kwa mujibu wa Katiba ili kutangazwa mshindi.
Mwenyekiti wa IEBC, Chebukati alimtangaza Dk Ruto kupitia Muungano wa Kenya Kwanza mshindi baada ya kupata kura 7,176,141 sawa na asilimia 50.49 huku Raila Odinga kupitia Muungano wa Azimio akipata kura 6,942,930 sawa na asilimia 48.85.
Wagombea wengine walikuwa ni Profesa George Wajackoyah kupitia chama cha Roots na kupata kura 61,969 sawa na asilimia 0.44 huku David Waihiga wa Chama cha Agano akipata kura 31,987 (0.23%).