Mahakama yazuia mauzo ya shamba la ekari 200

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi imetoa amri ya zuio la muda la kuuza shamba la ekari 200 lililopo katika eneo la Disunyara, Mlandizi mkoani Pwani.

Amri hiyo ilifuatia maombi yaliyofunguliwa Mei 24, 2023 na mmiliki wa shamba hilo, Richard Rweyongeza kwa hati ya dharura iliyoambatana na hati ya kiapo kupitia mawakili wake, Mpaya Kamara na Edward Chuwa.

Maombi hayo yalifunguliwa dhidi ya African Banking Corporation (T) Limited (ABC), kampuni ya Nutmeg Auctioneers & Property Managers Co. Limited na kampuni ya Inter 33/34 Limited.

Katika maombi hayo, muombaji aliiomba mahakama itoe amri ya zuio la muda la kuuza shamba hilo kupitia zabuni iliyokuwa ifunguliwe jana majira ya saa 5:30 asubuhi mpaka pale pande hizo mbili zitakapokutana na kufikia mwafaka.

Akisoma uamuzi huo jana, Jaji wa Mahakama hiyo, Isaya Arufani alisema mwombaji alipeleka maombi hayo chini ya kifungu cha 68(e) cha sheria ya mashauri ya madai akiomba mahakama amri ya zuio la muda la shamba hilo ili lisiuzwe wakati wakisubiri pande zote kukutana.

“Baada ya kusikiliza mawasilisho ya mawakili wa mwombaji yaliyoungwa mkono na hati ya kiapo, mahakama imeona kwamba, kama ameleta kwa hati ya dharura na ukweli kwamba tenda (zabuni) ilitakiwa kufunguliwa ya uuzaji wa shamba hilo na ilidhamiriwa kufanyika leo (jana), saa 5:30, mahakama imeona kwamba kwa maslahi ya haki, uhitaji wa kutuma notisi kwa mujibu maombi kabla ya kutoa zuio la muda kama ilivyoainishwa katika kifungu xxxvii, kanuni ya nne ya sheria ya mashauri ya madai,” alisema.

Pia mahakama iliamuru amri ya kutouza shamba hilo mpaka pande zote zitakapokutana Juni 1, 2023 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Sakata hilo lilianzia kwa mwombaji kuchukua mkopo katika Benki ya ABC ambapo waliwekeana makubaliano ya kulipa dola laki mbili na endapo atashindwa kuna utaratibu utapaswa kufuatwa kabla ya kufika hatua ya kuuza shamba hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button