Majaliwa apokea magari 51 uboreshaji uhifadhi wa utalii

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea magari 51 ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa msaada wa dharura wa uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi wa Utalii Tanzania katika Hifadhi za Taifa Serengeti, Nyerere na Pori la Akiba Selous wenye thamani ya Euro milioni 20 sawa na Sh bilioni 56.

Mradi huo unahusisha ununuzi wa magari zaidi ya 60, ndege moja na helikopta moja kwa ajili ya kuimarisha doria, uanzishwaji wa benki za uhifadhi za jamii pamoja na kuboresha mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji 55 vinavyozunguka ya hifadhi hizo.

Majaliwa amepokea msaada huo wa magari 51 kutoka Serikali ya Ujerumani jana Dar es Salaam.

Alisema Serikali ya Tanzania inathamini na kutambua uungwaji mkono na Serikali ya Ujerumani kupitia Msaada wa Dharura wa uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi wa Utalii ambao utekelezaji wake ulisainiwa Oktoba 2021 na unatekelezwa kwa pamoja kati ya Tanapa, Tawa na shirika lisilo la Kiserikali la Frankfurt Zoological Society (FZS) kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na kueleza kuwa magari hayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa uhaba wa vitendea kazi.

Alisema lengo la mradi huo ni kusaidia shughuli muhimu za uhifadhi na kupunguza athari zilizosababishwa na janga la Covid-19 kwenye utalii na uhifadhi, jambo lililosababisha kadhia kubwa katika mapato yatokanayo na sekta ya maliasili na utalii.

Kadhalika, alisema Serikali ya Tanzania inashukuru kwa msaada wa fedha za nyongeza wa Euro milioni 15 zilizotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na athari za Covid-19.

Msaada huo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa wakati wa mazungumzo baina ya nchi hizo Oktoba 2021. “Nimejulishwa na timu ya wataalamu kutoka Tanapa, Tawa na KFW kwamba mradi huu kwa sasa uko katika hatua ya maandalizi,” alisema.

Majaliwa alisema miradi hiyo siyo tu inaimarisha uhusiano uliopo kati ya serikali hizo mbili katika kusaidia sekta mbalimbali, bali pia ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa siku zijazo kati ya Tanzania na Ujerumani kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa bioanuwai kwenye mifumo ikolojia ya maeneo ya hifadhi za taifa.

“Nachukua fursa hii kutoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi na Wakuu wa Mashirika ya Tanapa na Tawa kuhakikisha msaada huu wa vitendea kazi unaenda kufanya kazi zilizokusudiwa za uhifadhi wa maliasili na utalii na kwamba vitendea kazi hivi vitumike na kutunzwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya matumizi ya mali za serikali,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess alisema kwamba serikali yao itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu na amefurahi kukabidhi msaada huo wa magari 51.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana amesema utekelezaji wa mradi huo utaendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria kwenye maeneo yaliyoainishwa.

Habari Zifananazo

Back to top button