DAR ES SALAAM; Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kufanya mapitio ya vikundi vyote vya jogging katika halmashauri zao na waviweka kwenye mipango ya maendeleo.
“Nendeni mkawasikilize ili muwatambue, muwashike mkono na muwaongoze kushiriki katika kukuza uchumi wao binafsi kupitia miradi mbalimbali kwenye halmashauri,” amesema.
Amesema hayo leo Jumapili, Juni 16, 2024, wakati alipoongoza tamasha kubwa la jogging lililoandaliwa na kituo cha Televisheni na Radio cha EFM. Jogging hiyo ya Kilomita tano ilianzia katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe hadi Tangi Bovu mbezi na kurejea viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa vikundi vya jogging kote nchini kuendeleza vikundi hivyo na kwenda kuvisajili kwenye halmashauri zao, ili waweze kutengeneza mazingira ya kushiriki kwenye fursa nyingine za kiuchumi
“Mnaweza kutumia jogging yenu ambayo mmeisajili, kuwa kikundi cha ushirika, kikundi cha uwekezaji, kikundi cha biashara ikiwa mmejisajili kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya Utamaduni na Michezo ya kila halmashauri,” amesema.
Katika Hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan ni kuhamasisha Watanzania kushiriki katika mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa.
“Tuendelea kumuunga mkono Rais Dk Samia kwa kuunda vikundi mbalimbali vya michezo,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa madhara ya kutofanya mazoezi ni makubwa na takwimu za wizara hiyo hazioneshi mwenendo mzuri katika magonjwa ya moyo na kisukari
“Hata kama una kisukari au shinikizo la juu la damu, ukifanya mazoezi unazuia usiende katika hatari kubwa ikiwemo ya kukatwa viungo, kinga ni bora kuliko tiba,” amesema.