Majaliwa: Diaspora tangazeni fursa za Tanzania

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wana-diaspora wawe mabalozi wa kuitangaza Tanzania kokote waliko na wawe tayari kuainisha fursa zilizopo nchini.

Majaliwa alisema hayo jana alipokutana na wanachama wa Tanzanite ambayo ni Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Japan. Jumuiya hiyo ina wanachama ambao ni wafanyakazi, waliojiajiri na wanafunzi.

“Ninyi ni mabalozi wetu, itangazeni Tanzania na onesheni fursa zilizopo nchini ili tupate wawekezaji mahiri wenye mitaji ya kuja kuwekeza nyumbani,” alisema Majaliwa.

Aliwataka watambue fursa zilizopo nchini na kuzisemea vizuri ili iwe fursa ya kupata wawekezaji na ikibidi wafanye ubia na Watanzania.

“Wana-Diaspora tafuteni marafiki wa kwenda kuwekeza nyumbani kwenye sekta mbalimbali kama utalii, madini, viwanda. Tunawategemea ninyi katika kupata hawa wawekezaji ambao ni makini kwa sababu ninyi mnaishi nao, mnawajua zaidi,” alisema Majaliwa.

Aliwataka pia watumie Kiswahili kama njia ya kukuza ajira kwani nchi nyingine zimeona fursa hiyo na zimeamua kukiweka kwenye mitaala yao.

Aliwaeleza mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita ukiwamo uboreshaji katika sekta za elimu, afya, maji, nishati, usafiri na usafirishaji na miundombinu ya barabara na reli.

“Kwenye sekta ya afya, tumejenga zaidi ya vituo vya afya 670 ambavyo vina vyumba vya upasuaji, maabara, jengo la mama na mtoto, sehemu ya kutolea dawa na chumba cha kuhifadhia maiti.

“Katika kila halmashauri tumejenga hospitali, kila mkoa kuna hospitali na sasa hivi zipo pia hospitali za kanda ambazo zinatoa huduma za kibingwa,” alisema.

Alitoa mfano kwenye sekta ya maji kuwa serikali imejenga miradi mikubwa ya maji katika miji ya Bunda, Butiama, Bukoba, Tarime, Rorya ambayo yote inatumia maji ya Ziwa Victoria.

“Mradi mwingine wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Nzega, Tabora na Igunga wenye thamani ya shilingi bilioni 550 unaendelea vizuri. Pia tunao mradi wa maji wa miji 28 kwa ufadhili kutoka Benki ya Exim ya India, hii ni kwa sababu Mheshimiwa Rais Samia tangu akiwa Makamu wa Rais alianzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani na anaiendeleza kwa kasi,” alisema.

Kuhusu barabara, alisema serikali imekamilisha barabara kuu za kuunganisha mikoa isipokuwa barabara mbili tu.

“Tunaendelea kuunganisha wilaya kwa wilaya na tumeanzisha Tarura ili kuimarisha barabara za vijijini ambapo kwenye kila makao makuu ya wilaya wanapatiwa kilometa mbili za barabara ya lami,” alieleza.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Japan, Frank Semaganga alisema jumuiya hiyo yenye wanachama 400 ilianzishwa ili wasaidiane kuleta mshikamano na kuitangaza Tanzania.

Semaganga aliomba serikali iangalie uwezekano wa kuboresha mifumo ya uendeshaji kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili wana-diaspora wawekeze kwa kununua hatifungani pindi zinapotangazwa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wanaosoma Japan (TSJ), Eunice Likotiko aliiomba serikali iangalie namna ya kutumia vizuri ujuzi wa Watanzania wanaosoma nje ya nchi wanapohitimu na kurejea nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button