Majaliwa kuongoza matembezi Mlima Kilimanjaro

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi  matembezi ya kuhamasisha upandaji miti kuokoa Mlima Kilimanjaro yatakayofanyika geti la Marangu Kilimanjaro Mei 17, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Nessa Dobora Nyakisinda amesema katika kampeni ya ‘Okoa Mlima Kilimanjaro’ wanakusudia kupanda miti bilioni moja kufikia mwaka 2050.

Amesema wanataka kupanda miti kiasi hicho kwa kuwa mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la joto duniani yanasababisha barafu ya Mlima Kilimanjaro kuyeyuka kwa haraka sana.

Advertisement

“Watafiti wanasema miaka 30 au 50 inayokuja barafu tunayoiona leo hatutaiona tena, kwa hiyo ni jukumu letu Watanzania kuja pamoja kwa ajili ya kuokoa Mlima wa Kilimanjaro,”

Amesema wana mikoa minne watakayoanza nayo ndani ya miaka mitano ikiwa ni pamoja na Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Arusha.

Amesema Mlima Kilimanjaro ni chanzo cha maji, hewa nzuri na huvuta watalii zaidi ya 65,000 hivyo, wanahitaji kuendelea kuulinda kwa kupanda miti na kuongeza kuwa wataanza matembezi hayo kuanzia geti la Marangu hadi Mandara ambapo kutakuwa na km 5, 10 na 16 na kuwakaribisha Watanzania wote waweze kushiriki kwa gharama za Sh 35000.

Ofisa Hifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania ((TANAPA) Haika Bayona amesema kile ambacho Nessa wanakifanya ni suala kubwa na la msingi linalotakiwa kuungwa mkono na Watanzania.

“Tuunge mkono jitihada hizi za upandaji miti mtafurahia sana matembezi haya, tuige mfano ambao Rais Samia Suluhu Hassan alifika Kilimanjaro na kututangaza duniani,”amesema.

Amesema kuna kampeni ya kuupigia kura Mlima Kilimanjaro upate tuzo ya kivutio Bora Afrika na pia, hifadhi za taifa kumi zinawania tuzo nane.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *