Majaliwa: Tumsaidie Samia kupata wasaidizi waadilifu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan anaguswa na suala la maadili hasa kwa vijana.
Majaliwa amesema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi na waumini waliohudhuria mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu yaliyoandaliwa na taasisi ya Aisha Sururu Foundation (ASF).
“Tunapowahifadhisha Quran vijana wetu, tuhakikishe jambo hilo jema linakwenda sambamba na ujenzi wa misingi imara ya malezi itakayowafanya wawe raia wema, waadilifu na wazalendo kwa nchi yao. Tukiwa wazazi, walezi na walimu wa Quran, nitoe rai kwamba tunapotoka hapa hebu tujiulize ni kwa kiasi gani tunaizingatia hii Quran tukufu katika mwenendo mzima wa maisha yetu ya kila siku,”amesema na kuongeza;
“Pia tutamsaidia Mheshimiwa Rais kupata wasaidizi wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.”
Majaliwa alihimiza viongozi wa dini kila wanapopata nafasi kwenye mimbari wakemee ukatili wa kijinsia na wale wanaoenda kinyume na maadili na desturi za Kitanzania.
“Nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini muendelee kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda mila, desturi na tamaduni za Kitanzania hususan katika kipindi hiki tunachokabiliwa na wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili,” alisema.
Majaliwa alisema Tanzania inakabiliwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili na pia kumeibuka wimbi la vitendo vingine ambavyo vinakwenda kinyume na dini, mila, desturi na tamaduni za kitanzania.
“Ninampongeza sana Dk Aboubakar bin Zubeir, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kwa kulisimamia kidete suala hili ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo mahsusi kwa viongozi wote wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania kulikemea na kutolifumbia macho,”alisema.
Aliwaomba waumini hao waendelee kuiombea amani Tanzania kwani ikipotea mikusanyiko kama hiyo haitoweza kufanyika.
“Nasi tuendelee kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Majaliwa.
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dk Aboubakar bin Zubeir alimpongeza Mwenyekiti wa taasisi ya ASF, Aisha Sururu kwa kuandaa mashindano hayo kwa miaka 22.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Amana ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Aboubakar Athuman Ally alisema kwa mwaka huu wametenga shilingi bilioni 40 kwa ajili ya uwezeshaji wa vikundi na wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.
Akisoma risala ya ASF, Zainab Matitu Vulu alisema washiriki wa mashindano hayo wanatoka maeneo tofauti nchini ambao jumla yao walikuwa 600 kutoka mikoa 20 ya Tanzania bara na visiwani na baada ya mchujo waliofanikiwa kuingia fainali ni 77.