Majaliwa: Tunataka watoto wafikie ndoto zao

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameihimiza jamii iwalinde watoto wasome wafikie ndoto zao.

Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kuanzia ngazi ya elimu msingi hadi chuo.

Alisema hayo Ruangwa mkoani Lindi jana alipotembelea shule za sekondari za Lucas Malia na Mary Majaliwa.

Advertisement

“Wazazi hii shule ni yetu, watoto ni wetu ni lazima tuwalinde na kuchangia kasi ya maendeleo katika shule hii, tuwatembelee walimu wetu ili tuwatie moyo, tunataka watoto wasome ili wafikie ndoto zao,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuungana na wananchi kuimarisha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora na kutimiza ndoto zao.

“Rais Dk Samia anaweza sababu amekuwa kiongozi imara, ameendelea kusisitiza kuwa yupo pamoja nanyi,” alisema Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa.

Alisema pamoja na Rais Samia kuweka mkazo katika kuipa hadhi sekta ya elimu, pia amewekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike kwa kuweka sheria zitakazomwezesha mtoto wa kike kutimiza ndoto zake.

“Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais wetu Dk Samia anasimamia ubora wa elimu kwa watoto wote ikiwemo wa kiume, watoto wetu wa kike tumewawekea mikakati mahususi ikiwemo sheria kali kwa wanaotaka kumkwamisha na sisi tunazisimamia ili aanze darasa la awali mpaka atakapomaliza akiwa salama,” alisema Majaliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack alisema mkoa huo unatekeleza mpango mkakati unaofanyiwa mapitio kila mwaka ili kuona upungufu kwa lengo la kurekebisha walipokosea na kukuza ufaulu kwa shule mkoani Lindi.

Ameongeza kuwa kupitia mpango huo wamefanikiwa kupunguza daraja sifuri kwa asilimia 40 na daraja la nne kwa zaidi ya asilimia 45.

“Asilimia zaidi ya 50 ya waliomaliza mwaka jana wataenda kidato cha tano na tuna uhakika mtoto aliyemaliza kidato cha sita mkoani Lindi anakwenda chuo kikuu,” alisema mkuu wa mkoa.

Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa aliwataka wanafunzi wasome kwa bidii na wasijihusishe na makundi maovu na badala yake waweke malengo katika masomo yao ili watimize ndoto zao kielimu.

“Nawausia watoto wangu someni ili muweze kupata sifa za kuwa viongozi na kuajiriwa ili muweze kuitumikia nchi yetu, Mheshimiwa Rais Dk Samia amefanya mambo makubwa sana katika kuliinua taifa,” alisema Mary.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *