DODOMA: SERIKALI imetoa wito kwa taasisi za kifedha ikiwemo benki kutoa fusa mbalimbali ikiwemo mikopo kwa wananchi wenye hati za kimila za ardhi.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 30,2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete, aliyehoji mkakati wa serikali kusaidia wananchi hasa wa vijijini wenye hati za kimila za ardhi kupewa fursa ikiwemo mikopo katika taasisi za fedha wakitumia hati hizo, ambazo baadhi ya benki hazizithamini.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema hati zinazotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na hati za kimila za ardhi zote zinatambulika kisheria na zinaztoa fursa mwenye nayo kupata mkopo.
Hata hivyo amesema inawezekana baadhi ya taasisi kwa sababu zao binafsi zinakataa hati hizo, lakini kisheria zote zinatambulika, hivyo kushauri taasisi zote nchini kuendelea kutoa fursa kwa wananchi hao kupata stahiki ya mikopo.