Majaliwa: Watendaji dhibitini viashiria vya uvunjifu wa amani

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Majaliwa alisema lengo la agizo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu.

Alisema hayo Jumatano Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani.

“Hatuna budi kuitunza amani yetu kulingana na umuhimu wake kwani amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano,”alisema Majaliwa.

Alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa kutafuta na kudumisha amani na usalama.

Pia, alisema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua na tahadhari ili kuendelea kudumisha amani.

Alisema kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.

“Ni lazima tuendelee kuilinda amani nchini kwetu, Watanzania tuendelee kudhibiti yeyote mwenye nia ya kuiharibu amani yetu. Jukumu la kuilinda amani hii ni agenda yetu sote, tuitekeleze.”alisema Majaliwa.

Alitoa mwito kwa Umoja wa Mataifa (UN) kuendelea kuunga mkono ajenda za maendeleo nchini ili kuhakikisha umaskini haugawanyi jamii bali uwe chachu ya kutafuta njia bora ya kujinasua katika hali hiyo.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania, Zlatan Milisic aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kinara katika kudumisha amani katika nchi za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wataendelea kusimamia utunzaji wa amani tuliyonayo kwani ni tunu muhimu tuliyojaliwa nchini.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button