Majambazi yavunja maduka ya ‘mawakala’ na kupora mil 31.2/-

WATU wasiojulikana wamevamia na kupora Sh milioni 31.2 kwenye maduka ya huduma za kifedha katika soko la Kijiji cha Ntinachi lililopo Kitongoji cha Majengo Kata ya Nyawilimiliwa wilayani Geita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay ametoa taarifa hiyo juzi kwa waandishi wa habari na kueleza uhalifu ulifanyika Aprili 23, 2023 majira ya saa 9:00 alfajiri.

Alisema kabla ya kuvunja maduka hayo wahalifu hao waliowashambulia walinzi kwa silaha za jadi na mlinzi mmoja mwanaume (34) alijeruhiwa kichwani kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali.

“Mlinzi huyo alipatiwa matibabu na anaendelea vizuri na eneo la soko linalindwa na walinzi saba wa Kampuni ya Right Support Security,” alisema na kuongeza:

“Pale kwenye huduma za kifedha kulikuwa na mawakala wa M-pesa, CRDB, NMB na Airtel Money, maduka yalikutwa yamevunjwa na kuporwa fedha hizo tulizozitaja.”

Kamanda aliwataka wananchi kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kwenye maeneo yao ili kulishika mkono Jeshi la Polisi kwenye suala la ulinzi kwa sababu kuna wakati Jeshi la Polisi linachelewa kuarifiwa.

“Lakini pia hawa watu wa vibanda vya miamala ya simu, wajitahidi kuweka walinzi ambao wana viwango kwa sababu ya usalama,” alisema.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika na tukio hilo ili kuwachukulia hatua na kuhakikisha wanakata mnyororo mzima wa vijana wanaojihusisha na uhalifu.

Habari Zifananazo

Back to top button