Makungwi wadai mtoto achezwe kuanzia miaka 10

MAKUNGWI wa jadi mkoani Mtwara wamependekeza kuwa  watoto wa kike kuwacheza kuanzia umri wa miaka 10 kwani ni umri ambao watakuwa na akili timamu ya kuelewa mafunzo wanayopatiwa na makungwi hao (maarufu unyago).

Hayo yamesemwa wakati wa mafunzo ya siku moja kwa makungwi hao wa jadi kuhusu kujadiliana kwa pamoja na baina ya makungwi na wadau mbalimbali juu ya mpango mkakati kuhusiana na namna ambavyo unahitimishwa mradi wa miaka minne wa kuwezesha wasichana kupaza sauti na kujadili changamoto zao.

Mradi huo ulianzishwa mwaka 2021 na unahitimishwa Disemba 2024, unaoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii mkoani mtwara la SDA  juu ya utoaji wa elimu kwa makungwi kuhusu kuondokana na mila na desturi walizokuwa wakizitumia awali kabala ya mradi kuwafundisha watoto wa kike pia elimu ya afya kwa mtoto wa kike, ujasialiamali na mengine.

Advertisement

Mwenyekiti wa Shirika la Makungwi mkoani humo (maarufu Stadi Ang’avu za Msichana ), Veronica Joseph kutoka Halmashauri ya Mji Nanyamba amesema kupitia mapendekezo hayo itasaidia kuwarudisha miaka ya nyuma walikotoka ambapo ilikuwa haikubaliki mtoto wa kike kuchezwa kabla hajafikisha umri huo wa miaka 10.

Wakati huo iliaminika kuwa mtoto chini ya umri wa miaka 10 akienda jandoni hatoelewa atakachofundishwa kutokana na umri wake kuwa bado hauwezi kubeba majukumu hayo lakini hivi sasa baadhi ya wazazi wamekuwa na utamaduni wa kuwacheza watoto chini ya umri huo hivyo sasa tunarudi kule nyuma, tunapendekeza mtoto wa kike achezwe kuanzia umri wa miaka hiyo 10 siyo kinyume na hapo’’

Hata hivyo kwa sasa baadhi ya wazazi mkoani humo wamekuwa na utamaduni kuwacheza watoto hao chini ya umri huo kwa madai ya kuwa ni tamaa ya pesa bila kujali kile wanachotaka kuwabebesha watoto wao ni aina gani ya majukumu akiwa katika umri huo hivyo atakayebainika kwenda kinyume na mapendekezo hayo atachukuliwa hatua za sheria.

Mkurugenzi wa Shirika hilo la Sda, Thea Swai amesema wakungwi hao wamekuwa ni sehemu ya kuleta mabadiko katika changamoto walizokuwa wakizitatua kupitia mradi huo kwani kipindi wanapanga mradi waligundua kwamba mila na desturi ya unyago ni  moja ya jambo lililolalamikiwa kuwa makungwi wamekuwa wakitoa mafunzo yaliyopitwa na wakati yasiyoweza kumjenga mtoto wa kike katika kuendana na karne ya 21 ya sanyansi ya tekinolojia inayolenga masuala ya elimu.

‘’Tulipoanza huu mradi tulishirikiana na makungwi kuona namna ya kuweka mtaala mmoja wa kufundishia katika unyago badala ya kufundisha zile mada za namna ya kutekeleza majukumu ya familia, kwa pamoja tumekubaliana sasa wanafundisha masuala ya heshima kwa walimu, wazazi’’

Ameongeza kuwa‘’Elimu ya mazingira, afya ya uzazi na mengine na mpaka sasa tumeweza kufikia makungwi zaidi ya 120 kutoka kata  50 tulizofanya kazi mwaka 2021-2024 na kuanzia mwaka 2025/28 tunafikiria angalau tufanye tena kata zingine 50 ili tuweze kuwafikia makungwi wengi zaidi’’amesema Swai.

Ofisa Utamaduni kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Fatuma Mtanda ‘’Kwa sasa unyago wetu una tafsiri moja na siyo pale mwanzo ulikuwa na tafsiri mbalimbali kwahiyo tumependa sana kitendo cha kufanya utafiti kwenye unyago wetu na kupata mtaala mmoja ambao sasa unatumika kwa watoto wetu wote, ni faraja kubwa na imetupa heshima kubwa kwakuwa sasa tutakuwa na kitu kimoja kinachofanana ’’anasema

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Thabitha Kirangi ametoa rai kwa makungwi hao kuwa, matarajio ya serikali ni kuona maarifa waliyoyapata wakati wa utekelezaji wa maradi yakajitokeze vizuri zaidi kuliko wakati wa mradi kwasababu tayari wameshaiva wanauelewa mzuri kuhusiana na masuala  mazima waliyojielekeza hivyo wakawe chachu kutokana na nafasi yao ni kubwa katika jamii.