Malezi bora tiba ukatili kwa watoto

WAZAZI wametakiwa kuhakikisha wanasimamia vyema malezi ya watoto ili kuwanusuru na masuala mazima ya vitendo vya ukatili ambayo vimekuwa vikitokea maeneo mbalimbali.

Hayo yameelezwa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Tomic Simbeye katika mkutano maalumu na wanafunzi na wazazi uliofanyika shule ya msingi Jaranja iliyopo kata ya Tlawi wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara.

Simbeye amesema katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto ofisi yake imeendesha zoezi la kutembela kata zote na kukutana na wanafunzi na wazazi kuzungumza na kutoa elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Katika mkutano huo, alisema wazazi wanatakiwa watoe malezi kwa watoto katika mazingira ambayo yana ukaribu ili kuweza kutoa nafasi kwa mtoto kueleza changamoto anazozipitia jambo ambalo litasaidia kufichua endapo kuna masuala ya ukatili ambayo yamemkumba.

“Tumezungumza na wazazi na kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali ambapo tumewaelimisha kwa kina juu ya malezi sahihi kwa watoto na wanafunzi na itawawezesha kusaidia kwa kiasi fulani kujua masuala ambayo yanamkumba mtoto.” amesema Simbeye.



